Na Mwandishi Wetu-New York,Marekani
TANZANIAna Kanada zimejadili fursa za kuimarisha ushirikiano katika kukuza haki, ujumuishwaji na ustawi wa watu wenye ulemavu katika kikao cha pande mbili kilichofanyika leo Juni 10, 2026 katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa New York, Marekani, pembezoni mwa Mkutano wa 19 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu (COSP19).
Kikao hicho kiliwakutanisha Naibu Waziri wa Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi na Katibu wa Bunge anayeshughulikia Masuala ya watu wenye Ulemavu Mhe. Leslie Church kutoka Kanada pamoja na viongozi na wataalamu mbalimbali wa masuala ya watu wenye ulemavu kutoka pande zote mbili.
Akizungumza katika kikao hicho,Mhe. Mahundi ameeleza kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imeweka kipaumbele katika kujenga taifa jumuishi ambapo watu wenye ulemavu wanatambuliwa kama wadau muhimu wa maendeleo na wanapewa fursa sawa katika elimu, afya, ajira na kinga ya jamii.
Pia, Pande hizo mbili zilijadiliana kuhusu namna ya kuimarisha ajira kwa watu wenye ulemavu, ambapo Tanzania ilieleza utekelezaji wa Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2010 inayotaka waajiri wenye wafanyakazi 20 au zaidi kuhakikisha angalau asilimia tatu ya watumishi wao ni watu wenye ulemavu na wenye sifa stahiki.
Kwa Upande wake, Mhe.Leslie Church ameishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania juu ya Uimarishwaji wa mifumo ya kinga ya jamii, uwezeshaji wa kiuchumi kwa watu wenye ulemavu na utoaji wa elimu kwa umma juu ya aina zote za ulemavu na uwezo wa kundi hili, hali itakayosaidia kuepuka unyanyapaa kwa watu wenye ulemavu ili kuimarisha maisha huru na kuongeza fursa za kiuchumi kupitia mafunzo ya ujuzi, mikopo na programu za kinga ya jamii.
Katika majadiliano hayo, Tanzania na Kanada zilionesha nia ya kuendelea kushirikiana katika maeneo ya uboreshaji wa sheria na viwango vya upatikanaji wa huduma kwa watu wenye ulemavu, ukusanyaji wa takwimu, utekelezaji wa sera na sheria za watu wenye ulemavu pamoja na programu za ajira jumuishi.
Kikao hicho kilihitimishwa kwa pande zote mbili kueleza utayari wa kuimarisha ushirikiano na kubadilishana uzoefu ili kuhakikisha haki za watu wenye ulemavu zinatambuliwa, kulindwa na kutekelezwa kikamilifu kwa manufaa ya jamii jumuishi na endelevu



0 Comments