MABORESHO YA MFUMO WA BOS YAIVUSHA BRELA KUTWAA TUZO SABASABA


Na Asha Mwakyonde, DAR ES SALAAM

WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA),umeendelea kuthibitisha nafasi yake katika kuboresha mazingira ya biashara nchini baada ya kutunukiwa tuzo ya Taasisi Bora kwa Kuwezesha Biashara katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), ikiwa ni matokeo ya jitihada zake za kuboresha huduma na kurahisisha usajili wa biashara kwa wananchi.

Tuzo hiyo imetolewa Julai 13, 2026, wakati wa hafla ya kufunga maonesho hayo iliyofanyika katika Uwanja wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere jijini Dar es Salaam. Tuzo hiyo ilikabidhiwa mbele ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA ambaye pia ni Meneja wa Sehemu ya Alama za Biashara na Huduma kutoka Kurugenzi ya Miliki Ubunifu, Seka Kasera, amesema ushindi huo unaonyesha kuwa maboresho yaliyofanyika katika mfumo wa BRELA Online System (BOS), yamekubalika na kupongezwa na wadau pamoja na wananchi.

Amesema maonesho ya mwaka huu yalikuwa ya kipekee kwa BRELA kwa kuwa yalitoa nafasi ya kusikiliza maoni ya wateja na kutambua mahitaji yao, huku taasisi hiyo ikiendelea kuboresha huduma zake ili ziendane na matarajio ya wafanyabiashara na wawekezaji.

“Tumeyapa uzito mkubwa maonesho haya kama ilivyo kwa miaka yote kwa sababu ndiyo hutupa fursa ya kufahamu mahitaji ya wateja wetu. Tunafurahi kuona wananchi wamepokea vizuri maboresho ya mfumo wetu wa BRELA Online System (BOS), ambao umeboreshwa ili kurahisisha huduma na kuondoa changamoto zilizokuwepo awali,” amesema Kasera.

Ameongeza kuwa BRELA itaendelea kuimarisha mifumo yake kadri sheria na teknolojia zinavyoendelea kubadilika, kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma za kisasa, sahihi na zenye ufanisi.

Kasera pia amewashukuru wananchi waliotembelea banda la BRELA katika maonesho hayo kwa kuendelea kuamini huduma za taasisi hiyo, pamoja na kamati ya majaji kwa kusimamia mchakato wa tathmini kwa kuzingatia uwazi na vigezo vilivyowekwa.

Katika kipindi chote cha maonesho hayo, BRELA ilifanikiwa kuwahudumia zaidi ya wafanyabiashara 1,200 kutoka maeneo mbalimbali nchini kwa kutoa huduma za usajili wa biashara na leseni papo kwa hapo, pamoja na elimu kuhusu huduma zake kwa makundi mbalimbali, ikiwemo vijana na wanawake.

Katika kundi la taasisi zinazowezesha biashara nchini, BRELA ilishika nafasi ya tatu. Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) iliibuka mshindi wa kwanza, huku Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ikishika nafasi ya pili.

Post a Comment

0 Comments

SERIKALI IMETENGA BILIONI 1 UKARABATI MAKAZI YA WAZEE NCHINI - NAIBU WAZIRI MAHUNDI