📍Yaweka msisitizo matumizi ya ADR katika biashara na jamii
Na Asha Mwakyonde, DAR ES SALAAM
MIGOGORO ni sehemu ya maisha na shughuli za kila siku, lakini namna inavyoshughulikiwa ndiyo huamua kama itakuwa chanzo cha maendeleo au hasara.
Wataalamu wa sheria wanaeleza kuwa utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala (Alternative Dispute Resolution – ADR) umeendelea kuwa suluhisho muhimu la kuharakisha upatikanaji wa haki, kupunguza gharama za mashauri na kudumisha mahusiano kati ya wahusika.
Mfumo huo unatajwa pia kuwa nyenzo muhimu ya kupunguza mlundikano wa kesi mahakamani na kujenga mazingira rafiki kwa uwekezaji na maendeleo ya biashara nchini.
Jitihada hizo zinatekelezwa kupitia Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi Tanzania (TIAC), taasisi huru iliyoanzishwa mwaka 2019 na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS),na kuzinduliwa rasmi Oktoba 2021.
Katika kipindi ambacho migogoro ya kibiashara, kifamilia na ya kijamii inaendelea kuongezeka sambamba na ukuaji wa shughuli za kiuchumi, wataalamu wa sheria wanaeleza kuwa utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala ambayo ni suluhisho linaloweza kuharakisha upatikanaji wa haki, kupunguza gharama za mashauri na kuimarisha mahusiano kati ya wahusika.
Mkurugenzi Mtendaji kutokaTIAC Magreth Magoma, akizungumza kuhusu mfumo huo katika utatuzi wa kwa upande wa kibiashara anaeleza kuwa Tanzania imeweka mfumo wa kisheria unaotambua na kusimamia ADR ili kuhakikisha wananchi na wafanyabiashara wanapata haki kwa haraka, kwa gharama nafuu na kwa ufanisi.
Anasema pamoja na mahakama kuendelea kuwa mhimili muhimu wa utoaji wa haki, utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala una faida nyingi zinazoufanya kuwa chaguo bora kwa wananchi, wafanyabiashara na taasisi mbalimbali.
"Mfanyabiashara anapokaa kwenye mgogoro kwa miaka mingi biashara yake husimama. Tunataka migogoro itatuliwe kwa haraka ili watu waendelee na shughuli zao kwa amani na kuchangia ukuaji wa uchumi," anasema.
Mkurugenzi Mtendaji huyo anaeleza kuwa moja ya sifa kuu za mfumo huo ni usiri, ambapo migogoro hushughulikiwa kwa faragha na taarifa hubaki kati ya wahusika isipokuwa pale wanapokubaliana vinginevyo.
Aidha, anafafanua kuwa tofauti na mashauri ya mahakamani ambako wahusika hawana nafasi ya kumchagua hakimu au jaji, katika mfumo wa ADR wahusika wanaweza kumteua msuluhishi, mpatanishi au mwamuzi mwenye utaalamu unaoendana na aina ya mgogoro unaowakabili.
"Migogoro ya biashara inaweza kutatuliwa na mtaalamu mwenye uzoefu katika sekta hiyo. Hii huongeza ufanisi na kuimarisha imani ya wahusika katika mchakato mzima wa utatuzi," anasema.
Anaeleza kuwa sheria za Tanzania zinatambua mbinu mbalimbali za utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala, zikiwemo maridhiano (reconciliation), majadiliano (negotiation), upatanishi (mediation) na usuluhishi wa kisheria (arbitration).
Kwa mujibu Magoma, hatua muhimu huanza wakati wa kuandaa mkataba, ambapo wahusika wanashauriwa kuweka kipengele kinachoeleza namna watakavyoshughulikia mgogoro endapo utatokea.
Anasema hata kama kipengele hicho hakikuwekwa kwenye mkataba, wahusika bado wanaweza kukubaliana baadaye kutumia utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala badala ya kufungua shauri mahakamani.
Magoma anabainisha kuwa lengo la mfumo huo si kutoa uamuzi pekee, bali kushughulikia chanzo halisi cha mgogoro ili wahusika waendelee kushirikiana bila kuendeleza uhasama.
"Unaweza kushinda kesi mahakamani lakini ukaondoka ukiwa umebaki na uadui. Katika utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala tunalenga kurejesha mahusiano mazuri na kujenga maridhiano ya kudumu," anssema.
CHANGAMOTO KUHUSU ADR
Akizungumzia changamoto zilizopo, anasema uelewa mdogo wa wananchi kuhusu mfumo wa ADR bado ni tatizo kubwa ambapo wafanyabiashara wengi wanaingia kwenye shughuli za biashara bila kuandaa mikataba rasmi.
Mkurugenzi Mtendaji huyo anasema hali hiyo husababisha ugumu wa kutatua migogoro inapojitokeza, kwa kuwa sheria inahitaji makubaliano ya kutumia utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala yawe yameandikwa.
"Biashara nyingi zinaanzishwa kwa kuaminiana tu bila mkataba. Migogoro inapozuka ndipo changamoto huanza. Ni muhimu makubaliano yawekwe kwa maandishi ili kulinda maslahi ya pande zote," anasema.
Anafafanua kuwa si kila mtu anaruhusiwa kutoa huduma za utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala, kwani sheria inamtaka anayefanya kazi hiyo kwa malipo apate mafunzo na kuthibitishwa na Wizara ya Katiba na Sheria.
Anaongeza kuwa masharti hayo yanawahusu wapatanishi, wasuluhishi, waamuzi pamoja na wawezeshaji wa majadiliano, ili kuhakikisha huduma zinazotolewa zinazingatia sheria na viwango vya taaluma.
UTOAJI ELIMU
Akizungumzia kuhusu utoaji wa elimu kwa Umma, anasema Chama cha Wanasheria Tanganyika kwa kushirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi Tanzania (TIAC), vinaendelea kuelimisha wananchi kupitia kampeni mbalimbali za msaada wa kisheria, ofisi za TLS zilizopo katika mikoa 21 nchini na ushiriki katika maonesho mbalimbali ikiwemo Sabasaba.
Magoma anawataka wananchi, wafanyabiashara na taasisi kuhakikisha wanatumia wataalamu wa sheria wakati wa kuandaa mikataba ili kulinda maslahi yao na kuweka utaratibu sahihi wa kushughulikia migogoro endapo itatokea.
"Mawakili wana utaalamu wa kuandaa mikataba inayolinda maslahi ya pande zote na kuweka mfumo mzuri wa utatuzi wa migogoro. Hii ni hatua muhimu katika kuzuia migogoro na kuhakikisha haki inapatikana kwa haraka," anasema.
Anasisitiza kuwa matumizi makubwa ya utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala yataendelea kuimarisha utoaji wa haki nchini, kupunguza mzigo wa mashauri mahakamani, kuhamasisha uwekezaji na kujenga mazingira ya amani na maendeleo ya uchumi.





0 Comments