Na Jackline Minja, WMJJWM
Mafinga - Iringa
SERIKALI itaendelea kuimarisha utoaji wa mafunzo ya ujuzi wa vitendo ili kuwawezesha wananchi, hususan vijana na wanawake, kujitegemea kiuchumi, kujiajiri na kuchangia maendeleo ya Taifa.
Naibu Waziri Mahundi ameyasema hayo Julai 12, 2026 alipozungumza na wanafunzi wa mafunzo ya muda mfupi ya cherehani pamoja na watumishi wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Kampasi ya Rungemba wilayani Mafinga , mkoani Iringa, ambapo amesema mafunzo hayo hayalengi kuwafundisha kushona nguo pekee bali kuwajengea uwezo wa kujitegemea, kuibua ubunifu na kutumia fursa zilizopo kuongeza kipato na kuboresha maisha yao.
Amesema katika kipindi ambacho ajira rasmi zimekuwa na ushindani mkubwa, mafunzo ya ujuzi wa vitendo ni nyenzo muhimu ya kuwawezesha wananchi kujiajiri, kuanzisha biashara zao na hata kuajiri wengine, huku akiwataka wanafunzi hao kutumia maarifa waliopata kwa kuzingatia ubora wa kazi, ubunifu na mabadiliko ya teknolojia ili kuzalisha bidhaa zenye ushindani katika soko.
"Wizara itaendelea kushirikiana na Chuo cha Maendeleo ya Jamii Kampasi ya Rungemba pamoja na wadau wa maendeleo kuhakikisha mafunzo ya ujuzi yanawafikia wananchi wengi zaidi na wahitimu wanaendelea kuungwa mkono kupitia fursa za masoko, mitaji na ushauri wa kibiashara ili waweze kuwa wazalishaji wenye tija na kuchangia maendeleo ya jamii."Alisema Naibu Waziri Mahundi.
Awali akisoma taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Chuo cha Maendeleo ya Jamii Kampasi ya Rungemba, mkuu wa Chuo hicho, Bw. Kidubya Kulamiwa amesema chuo kinaendelea kutekeleza jukumu lake la kutoa mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi, kufanya tafiti na kutoa ushauri elekezi kwa jamii.
Amesema mafunzo ya muda mfupi ya cherehani yamekuwa yakiwajengea wananchi ujuzi wa kujiajiri na kujiongezea kipato huku chuo kikiendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuimarisha maendeleo ya jamii.
Naye Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini Mhe. Dickson Lutevele (Villa) amewasihi wanafunzi wanaopatiwa mafunzo ya cherehani kuyatumia vizuri kwa kuanzisha shughuli za uzalishaji mali zitakazowaongezea kipato na kuwawezesha kutunza familia zao.
"Kwa sasa mimi mbunge wa eneo lenu nitaendelea kushirikiana na Serikali kwa kuhakikisha elimu ya ujuzi inawafikia wananchi wengi zaidi ili kuwawezesha kujitegemea kiuchumi na kuchochea maendeleo katika maeneo yao". alisema mhe. Villa
Kwa upande wao, wanafunzi wanaonufaika na mafunzo ya muda mfupi ya cherehani wameishukuru Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Shirika la SOS Children's Villages kwa kuwajali na kuwawezesha kupata mafunzo hayo yaliyowapa ujuzi wa kujitegemea ambapo elimu waliyoipata imewajengea matumaini ya maisha bora na wameahidi kuwa mabalozi wazuri kwa wenzao kwa kuwahamasisha kutumia fursa za mafunzo ya ujuzi na kujiepusha na vitendo vinavyosababisha mimba za utotoni ili waweze kutimiza ndoto zao na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii.





0 Comments