WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, ameitaka Bodi mpya ya pili ya Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) kuhakikisha uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika sekta ya uvuvi unatafsiriwa kuwa uzalishaji wa kibiashara, mapato na mchango mkubwa zaidi katika uchumi wa Taifa.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa bodi hiyo iliyofanyika leo Julai 13, 2026, katika Ofisi za Makao Makuu ya TAFICO, Ras Mkwavi, Kigamboni jijini Dar es Salaam, Waziri Dkt. Bashiru alisema Bodi hiyo inaanza kazi katika kipindi muhimu ambacho Serikali imeweka msisitizo mkubwa katika kukuza uchumi wa buluu kupitia uwekezaji wa kimkakati kwenye sekta ya uvuvi ikiwa ni utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050.
"Mnaanza kazi wakati ambao msingi wa uwekezaji umeanza kujengwa. Hivyo jukumu lenu ni kuhakikisha uwekezaji huo unazaa matokeo chanya ya kibiashara na ya maendeleo kwa Taifa," alisema Dkt. Bashiru.
Katika maelekezo yake, Waziri aliitaka Bodi kusimamia kwa karibu ukamilishaji wa miradi ya kimkakati ikiwemo uendeshaji wa meli ya uvuvi wa bahari kuu kwa utaratibu wa ubia (PPP), kuharakisha mabadiliko ya TAFICO kutoka hatua ya maandalizi kwenda uzalishaji halisi wa kibiashara, kupitia upya mpango mkakati na maandiko ya uwekezaji, kuimarisha upatikanaji wa rasilimali fedha, kujenga rasilimali watu yenye uwezo, kufanya maboresho ya muundo wa Shirika, kuendeleza ushirikiano na sekta binafsi pamoja na kuhakikisha uwazi, uwajibikaji na usimamizi wa mali zote za Shirika.
Akizungumza kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi, Mwenyekiti wa Bodi ya TAFICO Prof. Yunus Daud Mgaya, aliishukuru Serikali kwa kuiamini Bodi hiyo kuiongoza TAFICO katika kipindi cha miaka mitatu, akiahidi kuwa Bodi itafanya kazi kwa weledi, uwajibikaji na ushirikiano wa karibu na Wizara pamoja na Menejimenti ili kuhakikisha maelekezo yaliyotolewa na Waziri yanatekelezwa kikamilifu.
Awali akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo anayeshughulikia sekta ya uvuvi, Prof. Mohammed Sheikh, alisema sekta ya uvuvi inaendelea kuwa miongoni mwa sekta zenye mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi wa Taifa, huku Serikali ikiendelea kuwekeza katika miradi ya kimkakati ikiwemo Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko na kuimarisha Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) ili liwe chombo kikuu cha kuendesha uvuvi wa kibiashara nchini.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa TAFICO, CPA Shaibu Matessa, alisema Shirika limeingia katika hatua mpya ya maendeleo ambapo linaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati inayolenga kuifanya TAFICO kuwa taasisi ya kisasa ya kibiashara katika sekta ya uvuvi.
Uzinduzi wa Bodi ya Pili ya Wakurugenzi wa TAFICO unatarajiwa kuwa chachu ya kuimarisha usimamizi wa uwekezaji wa Serikali katika sekta ya uvuvi na kuhakikisha Shirika linafikia dhamira ya kuwa nguzo ya utekelezaji wa ajenda ya uchumi wa buluu kupitia uzalishaji, biashara na uendelezaji wa rasilimali za uvuvi kwa manufaa ya Taifa.
Sanjari na tukio hilo, Waziri Dkt. Bashiru amezindua maandalizi ya Kongamano la Kimataifa la Ukuzaji Viumbemaji Duniani (WA26T) na Ukuzaji Viumbemaji Afrika (AFRAQ26), ambapo Tanzania itakuwa mwenyeji wa Kongamano hilo litakalofanyika Desemba,2026 Jijini Dar es salaam.




0 Comments