TCAA YATOA FURSA KWA WADAU KUWASILISHA MAONI NA CHANGAMOTO

Na Asha Mwakyonde, DAR ES SALAAM

WANANCHI na wadau wa sekta ya usafiri wa anga wamehimizwa kutumia Dawati la Huduma kwa Wateja lililoanzishwa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA),ili kupata taarifa sahihi, kuwasilisha maoni na changamoto zao pamoja na kupata huduma kwa haraka na kwa ufanisi.

Akizungumza leo Julai 13,2026 katika banda la TCAA kwenye Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Afisa wa Dawati la Huduma kwa Wateja wa TCAA, Rashid Mngoya, amesema dawati hilo ni sehemu ya mkakati wa Mamlaka unaoongozwa na Mkurugenzi Mkuu, Dk.Jabiri Bakari, wa kuboresha huduma kwa wateja na kuimarisha mawasiliano kati ya TCAA na wananchi.

Amesema kupitia dawati hilo, wananchi na wadau wanaweza kupata maelezo kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na TCAA, kuwasilisha maoni na malalamiko yao pamoja na kuelekezwa kuhusu taratibu zinazohusiana na sekta ya usafiri wa anga.

Kwa mujibu wa Mngoya, dawati hilo limeanzishwa ili kuhakikisha kila hoja au changamoto inayowasilishwa inapokelewa, inafanyiwa kazi kwa wakati na mhusika anapatiwa mrejesho stahiki.

"Lengo letu ni kuhakikisha wateja wanapata huduma bora, sahihi na kwa wakati. Tunataka wananchi na wadau wawe na njia rahisi ya kuwasiliana na Mamlaka na kupata msaada wanaouhitaji," amesema.

Ameongeza kuwa TCAA itaendelea kusimamia sekta ya usafiri wa anga kwa kuzingatia weledi, uwazi na ufanisi huku ikihakikisha viwango vya kitaifa na kimataifa vya usalama, ulinzi na ubora wa huduma vinaendelea kuzingatiwa.

Kwa upande wake, Meneja Uhusiano wa TCAA, Ally Changiwa, amesema Mamlaka imeendelea kuboresha mifumo yake ya mawasiliano ili kurahisisha wananchi kupata taarifa na huduma.

Ameeleza kuwa moja ya maboresho hayo ni tovuti ya TCAA, ambayo sasa inapatikana kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza ikiwa na taarifa zilizoboreshwa na kuongezwa ili kuwafikia watumiaji wengi zaidi.

Aidha, amesema tovuti hiyo imeongezewa sehemu ya Maswali Yanayoulizwa Mara kwa Mara (FAQ), inayowapa wananchi majibu ya haraka kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na kusimamiwa na TCAA.

Amesema kupitia ushiriki wake katika Maonesho ya Sabasaba, TCAA inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu majukumu yake ya udhibiti wa usafiri wa anga, haki na wajibu wa abiria, matumizi salama ya ndege zisizo na rubani (drones), pamoja na huduma nyingine zinazohusu sekta hiyo.

Hatua hiyo inaonyesha dhamira ya TCAA ya kuendelea kuimarisha mahusiano na wadau, kuongeza uelewa wa umma na kuhakikisha huduma zake zinapatikana kwa urahisi, kwa lengo la kuendeleza sekta ya usafiri wa anga iliyo salama, yenye ufanisi na inayokidhi viwango vya kimataifa.

Post a Comment

0 Comments

WAZIRI DKT. BASHIRU AIAGIZA BODI MPYA YA TAFICO KUIGEUZA TAFICO KUWA INJINI YA UCHUMI SEKTA YA UVUVI