Dar es Salaam
NAIBU Spika wa Bunge Mheshimiwa Daniel Sillo amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS), Mheshimiwa Moussa Saleh Batraki pamoja na ujumbe wake ambapo wamejadiliana kuimarisha ushirikiano kati ya Bunge la Tanzania na OACPS.
Viongozi hao wamekutana leo Julai 21, 2026 katika Ofisi ndogo ya Bunge jijini Dar es Salaam
Mheshimiwa Sillo amesema Bunge la Tanzania litaendelea kushirikiana na OACPS na kwamba linaunga mkono juhudi zake katika kufanikisha malengo yake ya kikanda na Jumuiya kiujumla.
Aidha, amesema Bunge linaunga mkono juhudi na mageuzi yanayolenga kuifanya OACPS kuwa Jumuiya yenye ufanisi, uwajibikaji na uwezo wa kuhudumia nchi wanachama kutokana na nafasi yake ya kiungo muhimu cha kuimarisha ushirikiano kati ya nchi za Afrika, Karibiani, Pasifiki na Ulaya.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa OACPS, Mheshikiwa Batraki amelishukuru Bunge la Tanzania kwa nafasi yake kwenye Jumuiya na kwamba anaithamini Tanzania katika kuendeleza malengo ya OACPS na kuimarisha mshikamano wa nchi wanachama.
Mheshimiwa Batraki amesema ushiriki wa Bunge la Tanzania kwenye Jumuiya hiyo unaimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa kupitia sera na malengo ya Jumuiya hiyo katika kufikia maendeleo endelevu kwa manufaa ya nchi wanachama wa OACPS.
Kikao hicho kimehudhuriwa pia na Balozi wa Tanzania nchini Ubeligiji Mheshimiwa Jestas Nyamanga.





0 Comments