PSPTB YAZINDUA MAANDALIZI YA KONGAMANO LA WATALAAM WA UNUNUZI NA UGAVI SABASABA

📍Yahimiza wataalamu kuja na tafiti zenye ufumbuzi wa changamoto za ugavi

Na Asha Mwakyonde, DAR ES SALAAM

BODI ya Usajili wa Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB), imezindua rasmi maandalizi ya Kongamano la Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi litakalofanyika kuanzia Desemba 14 hadi 18, 2026 katika Hoteli ya Ngurdoto jijini Arusha, huku ikiwataka wataalamu na wadau wa sekta hiyo kujiandaa kushiriki kikamilifu.

Akizungumza katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF),'Sabasaba',  Mkurugenzi Mtendaji wa PSPTB, Godfred Mbanyi, amesema uzinduzi huo umefanyika katika banda la bodi lililopo ndani ya banda kuu la Wizara ya Fedha.

Mbanyi amesema mwaka huu ni wa kumi mfululizo kwa PSPTB kushiriki maonesho ya Sabasaba, ambapo wamepata fursa ya kuwahudumia wadau mbalimbali kwa kutoa elimu kuhusu usajili wa wataalamu, mitihani ya kitaaluma pamoja na majukumu ya bodi katika kuendeleza taaluma ya ununuzi na ugavi nchini.

Mkurugenzi Mtendaji huyo ameeleza kuwa kongamano la mwaka huu litafanyika kwa siku tano badala ya siku tatu kama ilivyokuwa awali, hatua inayolenga kutoa nafasi kubwa zaidi ya kujadili masuala yanayohusu maendeleo ya sekta ya ununuzi na ugavi.

Mbanyi amebainisha kuwa uamuzi wa kuhamishia kongamano katika Hoteli ya Ngurdoto umetokana na mahitaji ya wataalamu na wadau, akieleza kuwa mazingira ya eneo hilo yatawezesha kufanyika kwa mijadala yenye tija na kubadilishana uzoefu.

Amesema kongamano hilo litawakutanisha wataalamu wabobezi wa ununuzi na ugavi pamoja na wataalamu kutoka sekta nyingine, watakaowasilisha mada mbalimbali zikiwemo za maadili, afya na masuala mengine muhimu yanayochangia maendeleo ya taaluma hiyo.

"Mada kuu ya kongamano pamoja na orodha ya mada za mawasilisho zitakamilishwa na kuchapishwa kwenye tovuti ya bodi mwishoni mwa wiki hii ili kuwapa nafasi wataalamu wanaotaka kuwasilisha tafiti zao kujiandaa mapema," amesema.

Mbanyi amewataka waandishi wa mada kuwasilisha tafiti zenye ubora, zinazojikita katika hali halisi ya utekelezaji wa shughuli za mnyororo wa ugavi na kutoa mapendekezo ya kuboresha sekta hiyo, badala ya kuwasilisha maelezo ya kinadharia pekee.

Amesisitiza kuwa kongamano hilo linawalenga wataalamu wenye uzoefu mkubwa, hivyo mawasilisho yanapaswa kuonyesha tafiti, ubunifu na mwelekeo wa maendeleo ya baadaye ya taaluma ya ununuzi na ugavi.

Aidha, amewahimiza wataalamu na wadau wanaohitaji taarifa zaidi kuhusu kongamano hilo kuwasiliana na Meneja wa Mafunzo na Makongamano wa PSPTB, Castro Komba, au kutembelea tovuti ya bodi kwa maelezo ya kina.

Mbanyi ametoa wito kwa wataalamu wote wa ununuzi na ugavi pamoja na wadau wa sekta hiyo kujitokeza kwa wingi kushiriki kongamano hilo, akisema litakuwa jukwaa muhimu la kujifunza, kubadilishana uzoefu na kujadili mustakabali wa taaluma ya ununuzi na ugavi nchini.

Post a Comment

0 Comments

SERIKALI IMETENGA BILIONI 1 UKARABATI MAKAZI YA WAZEE NCHINI - NAIBU WAZIRI MAHUNDI