PPRA YASHUKURU WATANZANIA, YAJIVUNIA TUZO YA MFUMO WA NeST


📍Yasema elimu ya ununuzi wa umma yazidi kuwafikia wananchi.

Na Asha Mwakyonde, DAR ES SALAAM

MAMLAKA ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), imewashukuru Watanzania pamoja na wadau wa sekta ya ununuzi na ugavi kwa kuendelea kuiunga mkono katika kutekeleza majukumu yake, hatua iliyochangia taasisi hiyo kupata tuzo katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba).

Akizungumza leo Julai 13,2026 katika maonesho hayo, Meneja wa PPRA Kanda ya Pwani, Vicky Mollel kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Dennis Simba, amesema tuzo hiyo ni matokeo ya juhudi za mamlaka hiyo katika kutoa elimu kuhusu ununuzi wa umma pamoja na matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa ununuzi wa umma wa NeST.

Amesema PPRA inaendelea kuthamini ushirikiano wa wananchi na wadau mbalimbali ambao umeiwezesha kufikisha elimu ya ununuzi wa umma kwa makundi tofauti ya jamii.

Aidha, ameeleza kuwa mafanikio hayo yanaenda sambamba na kutambuliwa kwa mfumo wa NeST kimataifa, ambapo hivi karibuni Mkurugenzi Mkuu wa PPRA aliwakilisha Serikali nchini Uswisi katika Jiji la Geneva kupokea tuzo iliyoutambua mfumo huo kuwa miongoni mwa mifumo 20 bora ya Serikali duniani.

Meneja huyo amesema mafanikio hayo yanaonesha namna Serikali inavyoendelea kutumia teknolojia kuimarisha uwazi, ufanisi na uwajibikaji katika shughuli za ununuzi wa umma.

Pia amewahimiza wananchi na wadau ambao bado hawajapata uelewa wa kutosha kuhusu huduma na fursa zinazotolewa na PPRA kujitokeza kupata elimu kupitia ofisi za mamlaka hiyo na majukwaa mbalimbali ya utoaji elimu.

Ameongeza kuwa PPRA itaendelea kutumia maonesho, semina na kampeni za uelimishaji kuwafikia wadau wengi zaidi ili kuongeza uelewa kuhusu sheria, kanuni na matumizi sahihi ya mfumo wa NeST katika ununuzi wa umma.

Post a Comment

0 Comments

SERIKALI IMETENGA BILIONI 1 UKARABATI MAKAZI YA WAZEE NCHINI - NAIBU WAZIRI MAHUNDI