VETA YANG’ARA SABASABA, YATUNUKIWA TUZO KWA UBUNIFU NA UJUZI WA KITAALAMU


 Na Asha Mwakyonde, DAR ES SALAAM

UBUNIFU, tafiti zenye kulenga kutatua changamoto za jamii pamoja na mchango wake katika kuendeleza ujuzi wa Watanzania vimeifanya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), kutambuliwa katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) baada ya kutwaa tuzo ya nafasi ya tatu katika kundi la Taasisi za Elimu ya Juu, Uwekezaji, Ujuzi na Utafiti.

Tuzo hiyo imekuja baada ya VETA kuonesha uwezo wake katika kutoa elimu ya ufundi stadi, kuendeleza ubunifu na kuonesha teknolojia mbalimbali zinazozalishwa kupitia tafiti zinazofanywa na taasisi hiyo.

Akizungumza baada ya kufungwa kwa maonesho hayo, Meneja wa Uhusiano wa VETA, Sitta Peter, amesema mafanikio hayo yametokana na mwitikio mkubwa wa wananchi waliotembelea banda la VETA na kupata elimu kuhusu fursa zinazopatikana kupitia mafunzo ya ufundi stadi.

Amesema katika kipindi chote cha maonesho hayo, VETA ilitumia fursa hiyo kuonesha bunifu mbalimbali zinazotokana na tafiti zinazolenga kutoa majibu kwa changamoto zinazolikabili Taifa katika sekta tofauti za uzalishaji na maendeleo.

Sitta amesema tafiti zinazofanywa na VETA hujikita katika mahitaji halisi ya jamii ili kuhakikisha zinatoa suluhisho zenye manufaa na zinazoweza kutekelezwa katika mazingira halisi.

Ameeleza kuwa elimu ya ufundi stadi ina nafasi kubwa katika kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira kwa kuwawezesha vijana na wananchi kupata ujuzi wa kujiajiri, kuanzisha shughuli za kiuchumi na kuongeza thamani katika uzalishaji wa bidhaa na huduma mbalimbali.

Aidha, amesema tuzo hiyo ni chachu kwa VETA kuendelea kuboresha mifumo ya mafunzo, kuimarisha ubunifu na kuongeza ubora wa bidhaa pamoja na teknolojia zinazotengenezwa na wahitimu na taasisi zake.

“Ukuaji wa biashara na viwanda unategemea uwepo wa nguvu kazi yenye ujuzi. Ndiyo maana tunaendelea kusisitiza mafunzo ya ufundi stadi na ujasiriamali ili wahitimu wetu wawe sehemu ya maendeleo ya uchumi wa Taifa,” amesema Sitta.

Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yameendelea kuwa jukwaa muhimu kwa taasisi mbalimbali kuonesha huduma, bidhaa, bunifu na fursa za uwekezaji kwa wananchi pamoja na wadau kutoka ndani na nje ya nchi.

Post a Comment

0 Comments

SERIKALI IMETENGA BILIONI 1 UKARABATI MAKAZI YA WAZEE NCHINI - NAIBU WAZIRI MAHUNDI