📍Abuni mashine za kuongeza thamani ya mazao
Na Asha Mwakyonde, DAR ES SALAAM
MHITIMU wa Chuo cha Ufundi Stadi Dar es salaam cha Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA),Ernest Maranya, amesema ubunifu wa teknolojia za ndani unaweza kuwa chachu ya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno na kuinua kipato cha wakulima na wajasiriamali nchini.
Hayo ameyasema leo Julai 12,3026 na Maranya, ambaye ni mwanzilishi wa kampuni ya Maranya Engineering and Metals Fabrication katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF),'Sabasaba' amesema kampuni yake imejikita katika ubunifu na utengenezaji wa mashine mbalimbali zinazorahisisha usindikaji wa mazao na kuongeza tija katika uzalishaji.
Amesema kampuni hiyo hutengeneza mashine za kukanga karanga, korosho, kahawa na mazao mengine, pamoja na mashine za kusafisha nafaka kama mahindi, maharage, mtama na ngano.
Kwa mujibu Maranya mashine hizo husaidia kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno, hususan katika maeneo yanayokabiliwa na changamoto ya unyevunyevu unaoweza kusababisha mazao kuharibika au kuathiriwa na sumu kuvu (aflatoxin).
"Mashine hizi zinamwezesha mkulima kuboresha ubora wa mazao yake, kuyaongezea thamani na kuyafikisha sokoni kwa bei nzuri zaidi, jambo linalochangia kuongeza kipato," amesema.
Ameongeza kuwa mashine za kukanga karanga zinachangia uongezaji thamani wa mazao kwa kuwezesha uzalishaji wa bidhaa mbalimbali badala ya kuuza mazao ghafi, hatua inayowaongezea wakulima na wajasiriamali mapato.
Mbali na hilo, ameeleza kuwa kampuni yake pia hutengeneza mashine za kumenya na kukata viazi vya vya chips zinazorahisisha kazi kwa wajasiriamali wanaojihusisha na upikaji wa chips, huku zikipunguza matumizi ya nguvu kazi na kuongeza uzalishaji.
Aidha, amesema pia amebuni majiko yanayotumia mkaa mbadala (charcoal briquettes), ambayo yanatumia nishati kwa ufanisi, hivyo kupunguza gharama za upishi na kuchangia utunzaji wa mazingira.
"Mkaa huu hudumu kwa muda mrefu, hivyo mtumiaji anaokoa gharama za nishati huku akichangia uhifadhi wa mazingira," amesema.
Pia amesema kampuni yake imebuni bidhaa za tiba na kinga dhidi ya magonjwa mbalimbali ya ngozi yanayosababishwa na fangasi, zikiwemo fangasi wa miguu na sehemu nyingine za mwili.
Maranya amewataka wakulima, wajasiriamali na wananchi kwa ujumla kutumia teknolojia za ndani ili kuongeza thamani ya mazao, kuboresha uzalishaji na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika soko la ndani na nje ya nchi.
Aidha, amewakaribisha wananchi kutembelea ofisi za Maranya Engineering and Metals Fabrication zilizopo jijini Dar es Salaam ili kupata mashine na teknolojia mbalimbali zinazochochea maendeleo ya sekta ya kilimo na ujasiriamali.



0 Comments