Na Asha Mwakyonde, DODOMA
MWANAFUNZI kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), anayesomea Sayansi ya Chakula na Teknolojia, Fredrick Pius, ameibuka na bidhaa ya lishe iliyotengenezwa kwa kutumia mbegu za mchicha na mazao mengine ya asili, akisema ubunifu huo unalenga kupunguza utapiamlo, kuimarisha afya za watoto na kuongeza matumizi ya mazao yenye virutubisho ambayo hayatumiki kwa kiwango kikubwa nchini
Akizungumza Agosti 3,2026 katika Maonesho ya 33 ya Wakulima Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Dk. John Malecela, Nzuguni jijini Dodoma, Pius amesema bidhaa hiyo imetengenezwa kwa kutumia mbegu za mchicha kama kiungo kikuu, huku ikichanganywa na mbegu za maboga, mtama mweupe na viazi vyenye rangi ya chungwa ili kuongeza thamani ya lishe.
Amesema amechagua mbegu za mchicha kwa kuwa zina kiwango kikubwa cha protini, kinachofikia kati ya asilimia 14 hadi 17, pamoja na kuwa na asidi muhimu za amino ambazo hazipatikani kwa wingi katika nafaka zinazotumika mara kwa mara kama mahindi na ulezi.
Pius ameeleza kuwa mbegu hizo pia zina madini ya chuma (iron) ambayo husaidia kukabiliana na tatizo la upungufu wa damu, hususan kwa watoto wenye anemia, pamoja na madini ya kalsiamu na magnesiamu yanayochangia ukuaji imara wa mifupa kwa watoto na watu wazima.
Ameongeza kuwa bidhaa hiyo imeongezewa viazi vyenye vitamini A kwa ajili ya kuboresha afya ya macho na ukuaji wa watoto, huku mbegu za maboga zikichangia protini na mafuta yenye afya ambayo huongeza nguvu na kusaidia ukuaji bora wa mtoto.
Kwa mujibu wa Pius, lengo la kushiriki Maonesho ya Nanenane ni kuitambulisha bidhaa hiyo kwa jamii na kuhamasisha matumizi ya mazao ya asili ambayo mara nyingi hupuuzwa licha ya kuwa na virutubisho muhimu kwa afya.
Amesema matumizi ya mazao hayo yanaweza kuwa sehemu ya suluhisho la kupunguza utapiamlo nchini, kuboresha lishe ya watoto na kuongeza thamani ya mazao yanayozalishwa na wakulima wa Tanzania.
Pius amewahimiza wananchi kuzingatia matumizi ya vyakula vya asili vyenye virutubisho vingi ili kujenga jamii yenye afya bora na kuchangia mapambano dhidi ya utapiamlo.


0 Comments