TMDA YATOA MWONGOZO WA DAWA SALAMA KWA WAKULIMA NA WAFUGAJI NANENANE

Na Asha Mwakyonde, DODOMA 

MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA),imesema usalama,ubora na ufanisi wa dawa za mifugo, vifaa tiba na vitendanishi ni msingi muhimu wa kulinda afya ya mifugo na kuongeza tija katika sekta ya kilimo na mifugo, huku ikitoa wito kwa wananchi kutumia Maonesho ya Nanenane kupata elimu kuhusu matumizi sahihi ya bidhaa hizo.

Akizungumza katika Maonesho ya Kitaifa ya Nanenane yanayofanyika katika Viwanja vya Dk.John Malecela, Nzuguni jijini Dodoma, Meneja wa TMDA Kanda ya Kati Sonia Mkubwa, amesema mamlaka hiyo imeshiriki maonesho hayo kwa lengo la kutoa elimu kwa wakulima, wafugaji na wananchi kuhusu majukumu yake ya kusimamia ubora, usalama na ufanisi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi.

Amesema Kanda ya Kati inasimamia mikoa ya Dodoma, Singida, Morogoro na Iringa, hivyo maonesho hayo ni fursa muhimu ya kuwafikia wananchi wengi kwa wakati mmoja.

"TMDA ina jukumu la kuhakikisha dawa za mifugo, vifaa tiba na vitendanishi vinavyotumika nchini vina ubora, usalama na ufanisi. Tunatoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya bidhaa hizo ili kulinda afya ya mifugo na watumiaji," amesema Mkubwa.

Ameeleza kuwa mamlaka hiyo pia huhakikisha dawa zote zinazoingizwa nchini zimesajiliwa na zinakidhi viwango vya kitaifa na kimataifa, huku viwanda vinavyozitengeneza vikizingatia kanuni za uzalishaji bora (Good Manufacturing Practices - GMP).

Aidha, amesema maabara za TMDA zinatambuliwa kimataifa na hufanya uchunguzi kwa kuzingatia viwango vinavyokubalika duniani, jambo linaloongeza imani katika matokeo ya vipimo vinavyofanywa nchini.

Mkubwa ameongeza kuwa TMDA hufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika maeneo yanayozalisha, kuhifadhi na kusambaza dawa pamoja na kuhakikisha watoa huduma wana sifa na weledi unaohitajika.

Pia amesema mamlaka hiyo inaendelea kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vya ndani vya kuzalisha dawa, vifaa tiba na vitendanishi ili kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi.

"Tunawakaribisha wawekezaji wote wenye nia ya kuanzisha viwanda vya dawa, vifaa tiba au vitendanishi kufika katika ofisi za TMDA ili wapate ushauri wa kitaalamu kuanzia hatua za awali za maandalizi ya michoro ya viwanda hadi mchakato wa usajili," amesema.

Amesisitiza kuwa kuongezeka kwa viwanda vya ndani kutasaidia kuongeza upatikanaji wa bidhaa salama na zenye ubora, kuchochea ukuaji wa uchumi na kuongeza ajira kwa Watanzania.

Post a Comment

0 Comments

ZAIDI YA WATU 186 WANUFAIKA NA HUDUMA YA KUPUNGUZA UZITO KWA NJIA YA PUTO MLOGANZILA