BRELA KUSHIRIKISHWA KUBORESHA UTEKELEZAJI WA KATAZO LA BIASHARA KWA WAGENI

Na Mwandishi wetu 

WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) ni miongoni mwa taasisi zinazotakiwa kushirikiana katika kuboresha utekelezaji wa katazo la biashara 15 ambazo haziruhusiwi kufanywa na wageni nchini, baada ya Serikali kuanzisha tathmini ya pamoja kufuatia maoni na malalamiko ya wadau.

Tathmini hiyo imefanyika kupitia kikao kazi kilichoongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Balozi Waziri Rajab Salum, Septemba 16, 2026, kikihusisha taasisi mbalimbali zinazowezesha na kusimamia shughuli za biashara nchini.

Mbali na BRELA, kikao hicho kimewakutanisha Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (TISEZA), Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), Tume ya Ushindani (FCC), Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Idara ya Uhamiaji na Idara ya Kazi na Ajira kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu.

Wizara ya Uchukuzi pamoja na Halmashauri za Dar es Salaam na Mwanza nazo zilishiriki katika majadiliano hayo yaliyolenga kubaini maeneo yanayohitaji maboresho katika utekelezaji wa katazo hilo.

Balozi Waziri ameeleza kuwa hatua hiyo imechukuliwa baada ya Serikali kupokea maoni na malalamiko kutoka kwa wadau mbalimbali kuhusu utekelezaji wa katazo hilo, hivyo kuona umuhimu wa kufanya tathmini ili kuhakikisha utekelezaji wake unaendana na malengo yaliyokusudiwa.

Amebainisha kuwa Serikali inalenga kulinda na kuimarisha sekta ya biashara nchini kwa kuweka misingi imara ya kiuchumi na kujenga mazingira yatakayowawezesha Watanzania kunufaika kikamilifu na fursa za biashara.

Aidha, amesisitiza kuwa utekelezaji wa sheria na taratibu hizo unapaswa kuzingatia utu, akieleza kuwa pamoja na Serikali kuwa na wajibu wa kusimamia na kutekeleza sheria, hatua zinazochukuliwa hazipaswi kusababisha usumbufu usio wa lazima kwa wahusika.

Baada ya majadiliano na tathmini, kikao hicho kilipitisha mapendekezo yaliyofanyiwa maboresho, ambayo sasa yamewasilishwa kwa Waziri wa Viwanda na Biashara kwa ajili ya kutoa mwelekeo wa mwisho kuhusu hatua zinazofuata.

Hatua hiyo inalenga kuhakikisha utekelezaji wa katazo la biashara 15 unakwenda sambamba na sera, sheria na taratibu za Serikali, huku ukizingatia maslahi ya Taifa na kuhakikisha Watanzania wanapata nafasi ya kushiriki kikamilifu katika shughuli za biashara.

Kwa upande wa BRELA, ushiriki wake katika mchakato huo unaifanya taasisi hiyo kuwa sehemu muhimu ya utekelezaji wa maboresho yanayolenga kuweka ufanisi katika usajili wa biashara na utoaji wa leseni, kwa kuzingatia matakwa ya sheria na sera za Serikali.



Post a Comment

0 Comments

BRELA KUSHIRIKISHWA KUBORESHA UTEKELEZAJI WA KATAZO LA BIASHARA KWA WAGENI