Na Asha Mwakyonde
ULAJI bora ni ule unaozingatia ushauri wa wataalamu kwani kumekuwa na tabia ya watu kula vyakula bila kuzingatia mahitaji ya miili yao.
Wataalamu wanashauri kula vyakula kulingana na rika husika lakini pia kufanya mazoezi ili kujenga mwili na kuuweka sawa.
Tunapokula zaidi na hatufanyi mazoezi ya kujenga mwili, tunaweza kupata uzito au unene mwingi kupita kiasi.
Ofisa Lishe Mtafiti kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Abela Twin'omujuni anazungumzia ulaji unaofaa kwa kundi la vijana
balee anasema kulingana na tafsiri ya Shirika la Afya Duniani (WHO),kuna vijana balee wa kundi la kwanza ambao ni kuanzia umri wa miaka 10
hadi 19.
Ofisa huyo anafafanua kuwa kundi la vijana balee umri wa kwanza ni miaka 10 hadi 15 na umri wa mwisho ni miaka 15 hadi 19.
Twin'omujuni anaeleza kuwa lishe ni muhimu kwa kundi la vijana balee kwa sababu ni umri ambao ni kipindi cha pili cha ukuaji wa haraka
kinaotokea katika kundi hilo.
Anasema kipindi cha kwanza ni tangu mtoto akiwa tumboni hadi kufikia umri wa miaka miwili.
"Kutokana na ukuaji wa haraka unaotokea katika kundi hili wanahitaji chakula cha kutosha kutoka katika makundi matano ya chakula ili
kukidhi mahitaji muhimu ya miili yao ikiwamo, ukuaji wa kiali, kisaikolojia na kimwili, "anasema.
Anaongeza kuwa umuhimu wa lishe kwa vijana hao ni kukabili mahitaji mengine yanayowakabili mfano wanahitaji kupata viturubishi vya
vitamini na madini ambayo ni muhimu katika ukuaji wao.
Twin'omujuni anasema virutubishi hivyo vinapatikana kwenye vyakula
kutoka kundi la mboga mboga na matunda ambavyo vipo katika makundi
matano ya chakula.
Anafafanua kuwa kundi la kwanza ni nafaka, mizizi na ndizi ambalo linatoa kirutubishi kwa ajili ya kutia mwili nguvu.
Mtafiti huyo anabainisha kuwa kundi la pili ni la vyakula vya asili ya wanyama na jamii ya kunde kunde ambavyo hupatia mwili mafuta na kundi
la tatu ni mboga mboga za majani na zisizo za majani kama vile karoti na nyanya, kundi la nne ni matunda.
"Kundi hili la mboga mboga na matunda linasaidia katika kuupatia mwili vitamini na madini ambavyo husaidia kuimarisha kinga ya mwili,
huongeza hamu ya kula chakula na kusaidia ukuaji vizuri, "anasema.
Anasema vitamini hivyo na madini vinasaidia kwenye uwezo wa kujifunza na kuimarisha afya kwa ujumla ikiwemo ujenzi wa mifupa kupitia madini ya calcium.
"Tuna madini chuma ambayo yanasaidia katika utengenezaji wa damu na madini joto ambayo husaidia katika ukuaji mzuri wa kiakili, "anaeleza.
Anaongeza kuwa ili kijana awe na afya bora ni vizuri akala chakula kutoka katika makundi yote matano ya chakula bila kusahau maji ya kunywa.
Twin'omujuni anabainisha kuwa kundi la mwisho ni la mafuta, asali na sukari na kundi hilo linatakiwa kwa kiwango kidogo lakini lina umuhumu katika mwili.
"Lakini sambamba na makundi hayo matano tusisahau maji ya kunywa ambapo inashauriwa mtu kunywa kuanzi lita moja na nusu ila anaweza kunywa zaidi kulingana na shughuli anazozifanya, "anasema mtafiti huyo.
Anasema kazi za maji ni nyingi katika mwili ikiwamo kurekebisha joto la mwili, kusafirisha virutubishi ambavyo amevipata kwenye chakula.
Twin'omujuni anaeleza kuwa lishe bora kwa kijana balee inasaidia kuzuia uwezekano wa kupata magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza kama
vile magonjwa ya kisukari, shinikizo la damu la juu.
Anasema kijana anatakiwa kula vyakula kutoka kwenye makundi hayo ya chakula kwa kiwango sahihi kulingana na kazi zake anazozifanya ili
kuweza kuuweka mwili katika hali inayostahili.
kuweza kuuweka mwili katika hali inayostahili.
0 Comments