ALIYEHITIMU NIT ABUNI MASHINE YA KUCHAKATA MICHIKICHI


 Na Asha Mwakyonde,Dodoma

MHITIMU wa kozi ya  Uhandisi  Mitambo (Mechanical Engineering), kutoka Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Dionisia Fyuri amebuni mashine ya kuchakata michikichi kwa ajili ya kuzalisha mafuta ya mawese.

Ameiomba serikali na wadau wengine wa maendeleo kusaidia  upatikanaji wa fedha   kwa lengo la kusaidia Ubunifu huo ambao utawarahisishia wazalishaji wa mafuta ya mawese.

Akizungumza jijini Dodoma Aprili 27,2023 kwenye maonesho ya wiki ya Ubunifu Kitaifa (IWTZ), ambayo yanaendelea kufanyika katika viwanja vya Jamuhuri yenye kaulimbiu isemayo 'Ubunifu Kwa Uchumi Shindani', ameeleza kuwa wakati wa kumaliza masoma yake alibuni mashine ya kuchakata michikichi baada ya kuona inahitajika katika jamii hasa kwa wazalishaji wa mafuta hayo.

Mbunifu huyo amesema lengo la kubuni mashine hiyo ni kuweza kurahisisha hatua ambazo zinatumika wakati wa mchakato wa kupata mafuta hayo ambapo hutumia zaidi ya watu watatu ili kufanikisha upatikanaji wa mafuta hayo ikiwa ni pamoja na kuchukua muda mrefu.


"Niliona ni kazi kubwa kwa watu wa Kigoma ambao wanachakata mafuta haya ambapo huchukua muda mwingi pamoja na idadi kubwa ya watu wakati wa kuchakata mafuta ya mawese," ameeleza mbunifu huyo.

" Niilianza kwa nadharia niliandika kwa muda wa miezi minne na baadae nilianza kutengeneza kwa miezi minne tena hadi kukamilisha mashine hii," ameeleza mbunifu huyo.

Dionisia amewashauri vijana wenzake kujiunga na Chuo hicho kwani kuna kozi nyingi ambazo wanaweza kujifunza na kuweza kupata uelewa wa kubuni bidhaa wanazozitaka ambazo zitaenda kuisaidia jamii.

Ameongeza kuwa wasichana wanaosoma wasiogope kusoma masomo ya Sayansi inawezekana kwa wanafunzi wanawake huku akiwashauri wayasome kwa bidii ambapo yatawasaidia kupata fursa ya kusoma katika NIT.

Akizungumzia changamoto anazokabiliana nazo amesema hana kipato cha fedha ambacho kitamuwezesha kununua malighafi ili kutengeneza mashine hizo.

Post a Comment

0 Comments

 KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UTAWALA, KATIBA NA SHERIA YANOLEWA