BUNGE LAPITISHA BIL. 74.2 KUIMARISHA HUDUMA ZA MAENDELEO NA USTAWI WA JAMII MWAKA 2023/24


 Na WMJJWM,Dodoma

BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha bajeti ya shilingi Billioni 74.2 ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa mwaka 2023/24 leo Mei 18, 2023 jijini Dodoma.

Akiwasilisha Bajeti hiyo Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amesema vipaumbele vya Wizara ni pamoja na

kuratibu afua za kukuza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake kiuchumi (Generation Equality Forum - GEF) na kuratibu utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA).

Waziri Dkt Gwajima amesema kwa mwaka wa fedha 2023/24 Wizara itatekeleza Mpango wa Taifa wa kuhamasisha na kusimamia Maendeleo Ngazi ya Msingi, kukuza ari ya jamii kushiriki katika kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo na kutambua na kuratibu Makundi Maalum wakiwemo wafanyabiashara ndogondogo ili kuboresha mazingira ya biashara zao.

Waziri Dkt. Gwajima amesema pia Wizara itaboresha mazingira ya kufundisha na kujifunzia katika Taasisi ya Ustawi wa Jamii, Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru na Vyuo vya Maendeleo ya Jamii, kuratibu utoaji wa huduma za msingi kwa watu wenye mahitaji maalum ikiwemo huduma za msaada wa kisaikolojia kwa manusura wa majanga mbalimbali na makundi mengine yenye uhitaji katika jamii.

Amevitaja vipaumbele vingine kuwa ni kuratibu na kuwezesha upatikanaji wa haki za watoto na huduma za ustawi wa jamii kwa wazee, kuimarisha mifumo ya malezi, ulinzi na maendeleo ya watoto na familia na

kuimarisha utendaji kazi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ili mchango na ushiriki wa Mashirika hayo katika maendeleo ya Taifa uweze kutambulika na kuwa na tija kwa jamii. 

"Kwa upande wa shughuli za maendeleo, Wizara inakadiria kutumia Shilingi Billioni 30.5 kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo. Kati ya fedha hizo, Shilingi Billioni 26.8 ni Fedha za Ndani na Shilingi Billioni 3.7 ni Fedha za Nje. Kwa mwaka 2023/24, Wizara inaomba jumla ya Shilingi  Billioni 74.2 ili kutekeleza majukumu yake kwa maendeleo na ustawi wa jamii" amesema Waziri Dkt. Gwajima.

Post a Comment

0 Comments

 MAGARI 25 YA TUME YA MADINI YAMEZINDULIWA,YATASAMBAZWA KWENYE OFISI ZA MAAFISA MADINI