Dodoma
SERIKALI kupitia Wizara ya Madini, Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Chama cha Wazalishaji Chumvi Tanzania (TASPA) zimeanza kushughulikia changamoto za wazalishaji wa chumvi ghafi ili kuongeza uzalishaji na kuendeleza biashara ya chumvi nchini.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko leo Mei 18, 2023 jijini Dodoma, alipokutana na kuzungumza na wawekezaji, wazalishaji na wadau wa Sekta ndogo ya Chumvi ili kushughulikia changamoto zilizopo katika sekta hiyo.
Kufuatia hali hiyo, Dkt. Biteko ameunda Kamati Maalumu ya kupitia masuala yatakayoboresha Sekta ndogo ya chumvi na kuitaka kamati hiyo ndani ya siku Saba kutoa mapendelezo yatakayoboresha sekta hiyo.
Amesema, Rais Samia ametoa fursa kwenye Sekta ya Madini ili watanzania wanufaike na rasilimali madini na kuongeza kuwa Chama cha TASPA kuaminiana na kushirikiana ili kiwe imara katika kutekeleza shughuli zake.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesisitiza kuwa, wataalamu wa Sekta ya Madini wataendelea kupatiwa mafunzo mbalimbali yenye lengo ya kuwajengea uwezo katika usimamizi wa Sekta ndogo ya chumvi hapa nchini ili iwe na tija zaidi.
Akizungumza kwa niaba ya Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Viwanda Dkt. Yuda Benjamin amesema kuwa, Serikali inashughulikia changamoto za teknolojia ya uzalishaji na usafishaji wa chumvi ghafi ili kujenga Tanzania imara ya viwanda na kuinua uchumi wa nchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wazalishaji wa Chumvi (TASPA) Hawa Ghasia ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Madini na Wizara ya Viwanda kwa kuwakutanisha wadau wa Sekta ndogo ya Chumvi ili kushughulikia changamoto zao.
Naye, Mwakilishi wa chama cha TASPA Ally Ismail amesema sekta ya chumvi ni bidhaa muhimu sana katika afya kwa kuwa chumvi ni madini na chakula na kuiomba Serikali kuangalia soko la chumvi ili kupata soko la uhakika wa bidhaa hiyo muhimu.
Kikao hicho kimejadili changamoto mbalimbali zilizopo katika Sekta ndogo ya chumvi zilizowasilishwa na TASPA ikiwa ni pamoja na kupungua kwa biashara ya chumvi hapa nchini; uwepo wa Kampuni ya Neelkanth Salt Ltd ambayo inaingiza chumvi ghafi kutoka nje ya nchi; na kuendelea kutozwa kwa tozo zilizofutwa na kushuka kwa bei ya chumvi ghafi inayozalishwa nchini pamoja na kukosa soko la uhakika la chumvi ghafi inayozalishwa na wazalishaji wa ndani.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Kamishna wa Madini Dkt. Abdulrahman Mwanga, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi Yahya Samamba, wataalam wa Wizara na Taasisi, Maafisa Madini wa mikoa inayozalisha chumvi, wabunge, wazalishaji, wenye viwanda na wadau wa chumvi.
0 Comments