Na Asha Mwakyonde Dodoma
SERIKALI inaendelea kuratibu na kusimamia utoaji wa haki za msingi kwa mtoto pamoja na haki ya kuishi, kulindwa, kuendelezwa, kushiriki na kutobaguliwa.
Hayo yameyasemwa Mei 18,2023 Jijini Dodoma na Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum Dk.Dorothy Gwajima wakati akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024 ambapo kiasi cha shilingi bilioni 74.2 kimepitishwa na Bunge.
Waziri huyo amesema kuwa kutokana na upungufu wa watumishi hao kuna baadhi ya watoto hawazipati haki hizo ambapo wanaendelea wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo vitendo vya ukatili katika familia na jamii.
Ameongeza kuwa serikali kupitia wizara hiyo itaendelea kutekeleza maelekezo ya mamlaka na viongozi wa kitaifa katika kuhakikisha elimu inatolewa kwa jamii ili kudhibiti vitendo vinavyoashiria maadili yasiyofaa pamoja na mila na desturi zenye madhara kwa wanawake na watoto.
Aidha ameeleza kuwa moja ya sababu zinazosababisha ukatili dhidi ya watoto nchini ni mwendelezo wa mmomonyoko wa maadili katika jamii unaoambatana na mila na desturi za jamii husika ambazo zinasababisha ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto.
"Katika kushughulikia changamoto za vitendo vya ukatili dhidi ya watoto, Wizara kwa kushirikiana na Wizara nyingine za Kisekta imeendelea kuratibu na kusimamia utoaji wa elimu ya upatikanaji wa haki za watoto na kupinga ukatili dhidi yao kupitia makundi yote katika jamii," amesema Dk. Gwajima.
Amebainisha kuwa Katika kufikia kundi kubwa la watoto kwenye shule, Wizara imeratibu uundaji wa Madawati ya Ulinzi na Usalama wa Mtoto katika shule za msingi na sekondari likiwa ni jukwaa mahsusi la watoto la kutoa taarifa za viashiria na vitendo vya ukatili vinavyofanywa ndani na nje ya shule kwa usaidizi wa walimu wa malezi na unasihi.
Dk. Gwajima akizungumzia vipaumbele vya Wizara hiyo amesema kuwa ni pamoja na kuratibu afua za kukuza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake kiuchumi (Generation Equality Forum - GEF) na kuratibu utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA).
Ameongeza kuwa kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2023/24 Wizara hiyo itatekeleza Mpango wa Taifa wa kuhamasisha na kusimamia Maendeleo Ngazi ya Msingi, kukuza ari ya jamii kushiriki katika kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo na kutambua na kuratibu Makundi Maalum wakiwemo wafanyabiashara ndogondogo ili kuboresha mazingira ya biashara zao.
"Wizara itaboresha mazingira ya kufundisha na kujifunzia katika Taasisi ya Ustawi wa Jamii, Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru na Vyuo vya Maendeleo ya Jamii, kuratibu utoaji wa huduma za msingi kwa watu wenye mahitaji maalum ikiwemo huduma za msaada wa kisaikolojia kwa manusura wa majanga mbalimbali na makundi mengine yenye uhitaji katika jamii.
0 Comments