SERIKALI YATOA UFAFANUZI WA MABEHEWA YA TRENI NA NDEGE YA MIZIGO BADO IPO MIKONONI MWA MTENGENEZAJI

Na Asha Mwakyonde,Dodoma

SERIKALI  imesema kazi ya ukamilishaji wa mabehewa yanayoendelea kutengenezwa nchini Korea ambayo tayari mabehewa 14 mapya yalishafika na mengine 45 kazi inaendelea kukamilishwa.

Pia Watanzania wametakiwa kupuuza taarifa inayosambaa kwenye baadhi ya mitandao inayohusu  Sekta ya Anga Tanzania kukumbwa na kashfa nzito ya ndege yake ya mizigo aina ya Boeing767-300F kusafirisha mizigo haramu kwa njia haramu ambayo haijafuata taratibu za kiforodha.

Hayo yamesemwa Mei 31,2022 jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa  wakati akizingumza na Waandishi wa habari  amesema kuwa wanatarajia mabehewa yaliyobaki yatafika nchini wakati wowote ndani ya mwaka huu.

Msemaji huyo ameeleza kuwa kati ya mabehewa hayo  baadhi yake yameshakamilika na kati ya Juni 2-3, 2023 wanatarajia kupokea mabehewa sita ya ghorofa kwa ajili ya kutumika kwenye SGR.

"Mabehewa hayo yamefanyiwa ukarabati na kurejeshwa katika upya wake kwa zaidi ya asilimia 85, haya ni mabehewa ambayo yametoka Ujerumani ambapo jumla yake ni 30. Mabehewa 24 yataendelea kuja kwa awamu," amesema. Msigwa.

Akizungumzia kutokuanza kwa majaribio ya treni ya abiria kwa kipande cha kwanza cha reli ya kisasa ya SGR kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro ambayo imeshakamilika, kumesababishwa na kutokukamilika kwa wakati kwa utengenezaji wa vichwa vya treni viwili na mabehewa 30.


 Msigwa ameweka wazi sababu ya kutokukamilika kwa vichwa vya treni viwili na mabehewa 30 ni kutokana na changamoto katika upatikanaji wa baadhi ya vipuri vinavyotumika kwenye ukamilishaji wa vichwa vya treni ambavyo vinatoka nchini Canada ambako kutokana na changamoto ya UVIKO-19, vita na kuharibika kwa uchumi katika nchi nyingi duniani vimefanya viwanda vingi vinavyozalisha vipuri kutorudi katika ratiba za uzalishaji za kawaida. 

Ameongeza kuwa  Vipuri walivyotarajia vitafungwa kwenye vichwa viwili ni miongoni mwa vipuri ambavyo vimepata madhara kutokana na changamoto hizo hivyo, mtengenezaji hakuweza kuleta kwa muda aliopangiwa.

"Tumeshindwa kuanza majaribio kwa sababu hatuwezi kuyafanya kama vichwa vya kuvuta mabehewa havijafika, Serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu ukamilishaji wa vichwa hivi ili vitakapofika tuanze mara moja majaribio ya treni haya," ameeleza.

Amefafanua kuwa makubaliano mapya waliyoingia na mtengenezaji wa vichwa vya treni, ameahidi kichwa cha kwanza kitafika mwezi Julai na kikifika kitaanza majaribio mwezi huo huo na kwamba kichwa cha pili kitafuata . 

Msigwa amewatoa wasi wasi  Watanzania kwamba Serikali haijadanganya juu ya muda wa kuanza kwa majaribio ya treni hizo bali kilichotokea ni mabadiliko ya ratiba ya mtengenezaji yalioathiri kuja kwa vichwa hivyo.

Akitolea ufafanuzi kuhusu sekata ya Anga  Msigwa amesema Serikali inaona kwamba taarifa hizo ni za upotoshaji huku akisema  ni njia mojawapo ya kurudisha nyuma juhudi za Serikali  katika kukuza sekta hiyo na usafiri wa anga. 

Msigwa amesema Serikali inawafuatilia waliochapisha taarifa hiyo na hatua zitachukuliwa dhidi yao na kwamba 
Ndege ya mizigo aina ya Boeing767-300F bado haijafika Tanzania, haijaanza kazi rasmi, bado ipo mikononi mwa watengenezaji nchini Marekani na inatarajiwa kupokelewa nchini Juni 03 mwaka huu.

Post a Comment

0 Comments

 MAGARI 25 YA TUME YA MADINI YAMEZINDULIWA,YATASAMBAZWA KWENYE OFISI ZA MAAFISA MADINI