TANESCO YASAINI MKATABA WA BILIONI 275 WA KUZALISHA UMEME WA JUA


Na Asha Mwakyonde,Dodoma

WAZIRI wa Nishati January Makamba  ameshuhudia utiaji saini mkataba wa uzalishaji umeme kwa jua kwa kutumia Teknolojia ya Solar Photo Voltaic wenye uwezo wa kuzalisha megawati 150 za umeme.

Akizungumza jijini Dodoma Mei 29,2023 Waziri Makamba wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba wa kwanza nchini wa kuzalisha umeme wa jua wa Megawati 50 Kishapu mkoani Shinyanga,amesema kuwa serikali inaingiza hatua kubwa kwenye gridi ya Taifa.

Waziri huyo ameeleza kuwa baada ya miaka mingi ya matamanio  sasa ndoto imetumia huku akiwataka wananchi kukutunza mradi huo  wa uzalishaji umeme ambao utawapatia manufaa ya kuwapatia vijana ajira.


"Tunaanza safari zaidi ya kuzalisha umeme wa Nishati na umeme wa jua, TANESCO inatakiwa kuainisha maeneo ambayo yanaweza kuzalisha umeme wa jua na upepo," ameeleza Makamba.

Amesema serikali itaendelea kuyawezesha maeneo ambayo yapo mbali na gridi ya Taifa lengo likiwa ni kuhakikisha maeneo yote yenye vikwazo yanafikiwa ili kuwa na umeme wa uhakika.


Awali Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Maharage Chande ameeleza kuwa mradi huo una uwezo wa kuzalisha megawati 150 za umeme  na kwamba utatekelezwa kwa awamu mbili ambapo ya kwanza zitazalishwa megawati  50.

Mkurugenzi huyo amesema awamu ya pili itahusisha uzalishaji wa megawati 100 na kwamba mradi huo utatekelezwa na Kampuni ya SINOHYDRO CORPORATION kutoka nchini China na gharama za mradi hadi kukamilika ikiwamo kulipa fidia kwa wanaopisha eneo la mradi ni kiasi cha shilingi bilioni 274.76.

Ameongeza kuwa mradi huo unatarajiwa kuanza Juni mwaka huu ambapo utachukua muda wa miezi 14 hadi kukamilika.

"Kusainiwa kwa mradi huu ni sehemu ya mipango ya mapinduzi katika uzalishaji wa umeme kwa kutumia vyanzo mseto katika sekta ya Nishati nchini ili kufikia lengo la kuwa na megawati 5000 kwenye gridi ya Taifa ifikapo mwaka 2025," amesema Chande.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christine Mndeme amesema mradi huo watausimamia na kuutunza ili uweze kuwanufaisha   wananchi na Watanzania wote kwa kuwapatia ajira.

Ameongeza kuwa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amekuwa akiwapelekea fedha nyingi katika miradi mbalimbali  ya kimkakati mkoani huo.

"Tuna kila sababu ya kumshukuru Rais Dk. Samia ambaye amedhamiria kulipeleka Taifa mbele kiuchumi," ameeleza Mkuu huyo wa Mkoa.

Mradi huo ni mkubwa haukuwahi kutokea wa kuzalisha umeme jua kwa kutumia Teknolojia ya 'Solar Photo Voltaic' hapa nchini na katika ukanda wa Afrika Mashariki hivyo kwa mara kwanza Shirika hilo limeandika historia ya kusaini mkataba huo ambao umefadhiliwa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD).

Post a Comment

0 Comments

MAJALIWA: MJI KONDOA TUMEKUSANYA ZAIDI YA MILIONI 126 KIPINDI CHA JULAI HADI JUNI MWAKA HUU