Na WMJJWM, Dodoma
SERIKALI imesema itashirikiana na wananchi pamoja na wadau wote walio tayari kutokomeza vitendo vya ukatili ndani ya Jamii.
Kauli hiyo Imetolewa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima wakati akizindua Kampeni ya "ONGEA NAO" iliyoandaliwa na Jeshi la Polisi jijini Dodoma kwa kushirikiana na kituo cha redio cha AfM cha jijini Dodoma, Juni 03, 2023.
Mhe. Gwajima amesema pamoja na jitihada mbalimbali za Serikali za kuhimiza maadili mema na Upendo ndani ya jamii, bado kuna matukio mengi ya ukatili wa kijinsia katika familia na wahanga wakubwa ni wanawake na watoto.
Kwa mujibu wa taarifa ya makosa ya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji kutoka Jeshi la Polisi kwa Januari hadi Disemba 2022, jumla ya matukio ya ukatili kwa watoto yalikuwa 12,163 (wavulana 2,201 na wasichana 9,962) ukilinganisha na matukio 11,499 kwa mwaka 2021 sawa na ongezeko la matukio 664" amesema Dkt. Gwajima.
Ameongeza kuwa, ukatili wa kijinsia huchangiwa na kuporomoka kwa maadili na changamoto za kiuchumi ndani ya familia ambapo madhara mojawapo ni kupunguza nguvu kazi ya taifa, kuleta umasikini katika familia na kusababisha jamii kuishi kwa hofu hivyo ana imani baada ya uzinduzi wa kampeni hiyo jamii itapata elimu kuhusu ukatili wa kijinsia na kuchukua hatua ya kupunguza matukio ya ukatili.
Wakati huo huo Mhe. Gwajima ametoa rai kwa Wazazi na Walezi kuhakikisha wanawalinda na kuwathamini watoto, kuwa wepesi kutoa taarifa inapotokea au wanapokutana na vitendo vya ukatili wa kijinsia huku akiziasa baadhi ya jamii zinazoendeleza mila na desturi zenye madhara kwa jamii ukatili wa kijinsia kuacha.
Kwa upande wake Naibu Kamishna wa Polisi Maria Nzuki kutoka Kamisheni ya Jinsia amesema Kampeni hiyo inalenga kuisogeza jamii karibu na jeshi la Polisi ili kujenga uelewa wa kujua viashiria vya ukatili kabla haujatokea.
"Mradi huu utagusa maeneo mbalimbali nchini kwa kuanza na mkoa wa Dodoma. Uzinduzi huu ni mwanzo wa uzinduzi ndani ya mikoa yote nchini." amesema Maria Nzuki.
Naye Diwani wa kata ya Ihumwa ilipozinduliwa kampeni hiyo, Mhe. Edward Magawa amebainisha kwamba kampeni hiyo imekuja wakati muafaka ambapo kata hiyo ina miradi mingi ya Serikali, hivyo wageni ni wengi wakiwemo wahalifu.
"Kata yetu tumeamua kupinga vitendo vya ukatili kwa vitendo, ili kuliongezea nguvu jeshi la polisi, tumeamua kujenga kituo cha polisi cha kata ya Ihumwa." amesema Mhe. Edward.
0 Comments