BRELA YAWAHAMASISHA WADAU KUTEMBELEA BANDA LAO, IMEJIPANGA KUTOA HUDUMA

Na Asha Mwakyonde Dar es salaam

WADAU na wananchi wameshauriwa kupita katika mabanda ya Wakala ya Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA),yaliyopo katika Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), maarufu Saba Saba, yenye kaulimbiu isemayo "Tanzania Mahali sahihi pa Biashara na Uwekezaji" ili kupata huduma zinazotolewa na Wakala hiyo.

Akizungumza jijini Dar es salaam Julai 03,2023 katika maonesho hayo 
Mkuu wa Kitengo Uhusiano kutoka BRELA, Roida Andusamile amesema 
 kuwa kwenye maonesho ya mwaka huu wanamabanda manne ambapo kila moja linatoa huduma zake ambazo zinajitegemea.

Ameongeza kuwa wanatoa huduma mbalimbali katika mabanda yao ili wadau endapo watapata shida katika kusajili kwa njia ya mtandao wapate usaidizi huku akisema mbali na kupata usaidizi huo pia wanatoa elimu kwani baadhi ya wanajamii hawajui kazi ya BRELA.

"Tunashiriki maonesho haya ya biashara ikiwa ni mwendelezo wa kuhamasisha wadau mbalimbali na kuwahimiza kusajili alama za biashara, majina ya biashara, Usajili wa Kampuni, kupata Leseni ya biashara kundi A pamoja na Leseni ya viwanda," ameongeza.

"Tupo hapa  nje katika banda la Wizara ya Fedha na Mipango na banda letu limegawanyika katika sehemu mbili, banda la huduma za jumla na banda lingine linahusika na masuala ya miliki ubunifu, bado uelewa wake ni mdogo hivyo tumeona ni vizuri kuwa na banda maalumu ambalo litatoa elimu kuhusu masuala ya kibinifu," amesema.

Amefafanua kuwa kuna wavumbuzi wengi hapa nchini wanavumbua vitu mbalimbali lakini hawajui kulinda zile vumbuzi zao na kwamba mvumbuzi  anapolinda vumbuzi zake BRELA itamuwezesha kunufaika zaidi baada ya kusajili.


Mkuu huyo wa Kitengo ameongeza kuwa kuna wasomi wengi hapa nchini wamevumbua vitu mbalimbali lakini hawajui waende wapi hivyo  BRELA ipo kwa ajili yao kusaidia kusajili hizo vumbuzi zao ili waweze kunufaika nazo.

Amesema mbali na maonesho hayo wamekuwa wakipita katika mabanda mbalimbali kwa wadau ambao ni wanafunzi wanaohusika na vumbuzi kwa kuwa ni muhimu wakasajili vumbuzi zao.

Mkuu huyo wa Kitengo amesema wapo wavumbuzi ambao ni mashuhuda waliosajili vumbuzi zao ambapo kwa sasa wananufaika nazo.

Amesema pia wanabanda la kiliniki ya biashara ambalo lipo ndani ya banda la Kilimanjaro ambapo kuna mtaalamu anayetoa usaidizi kwa wanaopata changamoto kwenye mfumo na wanabanda ndani ya banda la Uwekezaji ,Viwanda na biashara na kwamba wanatoa huduma za papo kwa papo wadau wanaotembelea banda hilo wanapata huduma hizo.

Akizungumza na mara baada ya kukabidhiwa cheti cha alama ya biashara Afisa Uhusiano na Mawasiliano kutoka  Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Augustina Makoye amesema kuwa amefika katika banda la BRELA kwa ajili ya kufanya Usajili wa alama ya biashara ambayo bodi hiyo itakuwa ikiitumia katika shughuli zake za kutangaza utalii ndani na nje ya nchi.

"Katika upatikanaji wa huduma hii sikupata changamoto yoyote nimejaza fomu kupitia mtandaoni ( online),na nilipokuwa na changamoto nilipiga simu BRELA walinipatia ushirikiano hadi kukamilisha Usajili huu," ameeleza.

Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI