BRELA YAWASHAURI WAKULIMA, WAFUGAJI KUSAJILI ALAMA ZA BIASHARA

Na Asha Mwakyonde, Dodoma 

WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), umewashauri wakulima kusajili nembo na alama za biashara kwa kuwa wanazalisha bidhaa mbalimbali na kuzipeleka sokoni.

Akizungumza leo Agosti 4,2024 kwenye Maonesho ya Wakulima na Wafugaji Nanenane yanayofanyika kitaifa jijini Dodoma, Ofisa Usajili kutoka BRELA Dodoma, Gabriel Girangay, amesema wanaendelea kutoa elimu kwa wakulima na Wafugaji watambue kuwa BRELA ni muhimu kwao katika kusimamia, kulinda bidhaa zao. 

Afisa huyo ameeleza Wakulima na Wafugaji ni wadau muhimu kwa kuwa wanapozalisha mazao yao wanayaongezea thamani hivyo wanahitaji kusajiliwa nembo au alama za biashara.

Girangay ameongeza kuwa watalinda vumbuzi zao katika masuala mbalimbali yanayohusiana na kilimo pamoja na teknolojia.

Amesema wapo kwenye maonesho hayo kwa ajili ya kutoa elimu na huduma mbalimbali katika banda lao ambapo mtembealaji atapata huduma za kusajiliwa jina la biashara na kila Mtanzania mwenye nia ya kuanzisha biashara afike huku akisema kuna wataalam wa masuala ya Tehama, biashara, alama za biashara na huduma na shughuli zetu nyingi zinafanyika kidijitali. 

Amesema wakala huo unafanya kazi ya kusajili kampuni, majina ya biashara, alama za biashara na huduma, kutoa leseni za biashara kundi A, leseni za viwanda, kusajili viwanda vidogo na kulinda vumbuzi za wataalam mbalimbali.

“Tunatoa leseni za biashara kundi A ambazo ni zile zenye sura ya kitaifa na kimataifa, utaelimishwa kwanza na kama unataka kusafirisha bidhaa kwenda nje ya nchi au kutoa bidhaa kutoka nje na kuleta nchini utapata leseni BRELA,” amesema.

Kulingana na ofisa huyo, BRELA inatoa leseni za viwanda vikubwa na vya kati vyenye mtaji wa kuanzia Sh milioni 100 kwenda juu lakini Sh milioni 100 kwenda chini ni viwanda vidogo ambavyo pia wanavisajili. 

Aidha amesema kama mtu anahitaji kupata taarifa yoyote kuhusu kampuni, majina ya biashara, leseni au wanaotaka kukopa na kuingia ubia wa kibiashara afike katika banda hilo au ofisi za wakala huo na atapatiwa.

Post a Comment

0 Comments

MAJALIWA: MJI KONDOA TUMEKUSANYA ZAIDI YA MILIONI 126 KIPINDI CHA JULAI HADI JUNI MWAKA HUU