Na Asha Mwakyonde,Dodoma
MSAJILI wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania (TNMC),Agnes Mtawa amesema kuwa muuguzi, Mkunga akiweza kutekeleza misingi saba ya kanuni na maadili ya Uuguzi na Ukunga ataweza kutoa huduma iliyobora yenye staha na salama.
Hayo ameyasema leo Agosti 04, 2024 jijini hapa katika Maonesho ya Wakulima na Wafugaji (nane nane),yanayofanyika Kitaifa kwenye viwanja vya nane nane Nzuguni jijini Dodoma ameeleza kuwa katika taaluma wanahudumia watu wengi wa aina tofauti tofauti na kwamba kila sehemu ya huduma wauguzi na wakunga hao wapo.
Msajili hiyo ameeleza kuwa ili waweze kutoa huduma iliyobora wauguzi na wakunga hao lazima wazingatie msingi saba ya maadili yao.
Mtawa ameitaja na kufafanua misingi hiyo ambapo amesema ni lazima waheshimu utu, mila na desturi na kwamba wanapomhudumia magonjwa wamuhudumie kama yeye na sio kumlinganisha na mtu mwingine.
"Msingi mwngine ni lazima muuguzi, mkunga apate idhini ya mteja kabla ya kutoa huduma, magonjwa aelezwe anapata huduma gani na msingi wa tatu ahakikishe anawajibika na kile anachokifanya kama anampa dawa ahakikishe anafuata taratibu ili chochote kinachotokea awajibike mtoa huduma na si mtu mwingine," amesema Msajili huyo.
Amesema kuwa msingi wa nne ni lazima muuguzi, Mkunga afanye kazi kama timu ili magonjwa aweze kutibiwa na timu hiyo na kwamba msingi wa tano mtoa huduma atunze siri za magonjwa asiwe chanzo cha magonjwa huyo kushindwa kupata huduma.
Mtawa ameongeza kwamba msingi wa sita lazima muuguzi,mkunga awe tayari kujiendeleza kitaalamu kwa kuwa taaluma ya mambo ya afya inabadilika kila siku.
Amesema kuwa msingi wa saba muuguzi, mkunga anapaswa kuwa mwaminifu kutoa huduma bila upendeleo wa kuangalia rafiki,kabila na rangi ili kuleta usawa katika kuhudumia wagonjwa.
Awali Afisa Uhusiano wa Baraza hilo Ezekiel Nyalusi, amesema jamii ni vyema ikafahamu haki na wajibu wa mteja au mgonjwa pindi anapofika kupewa huduma za Afya katika kituo cha kutolea huduma.
Nyalusi ameziainisha haki hizo kuwa ni kupatiwa taarifa anazohitaji magonjwa kuhusu ugonjwa na matibabu yake, kupatiwa matibabu bila kukemewa, kukaripiwa au kufedheheshwa, Kupata huduma kwa wakati, kutegemea aina ya huduma.
Amesema haki nyingine ni kuwa na hiyari kupata taarifa za kiafya, kupata huduma stahiki kwa makundi maalumu kama vile, Walemavu, Wazee, Wajawazito, Watoto wa chini ya miaka mitano na wenye magonjwa sugu.
" Vile vile kulalamika au kutoa mrejesho wa huduma uliyopatiwa, kufuata kanuni na taratibu za kituo husika, kuwaheshimu watoa huduma ikiwa ni pamoja na kutumia lugha Safi, kumueleza muhudumu wa Afya taarifa zote ambazo zitamuwezesha kutoa tiba sahihi ikiwa ni pamoja na kumpa rekodi za matibabu ya awali alizonazo magonjwa," ameeleza .
Ameongeza kuwa haki nyingine ni kutafuta matibabu kwa haraka na mapema iwezekanavyo ili wahudumu wa Afya waweze kutoa huduma sahihi.
0 Comments