TARURA YAWEZESHA WAKULIMA KUSAFIRISHA MAZAO VIJIJINI

Na Asha Mwakyonde,Dodoma

WAKALA wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA),umesema kuwa umeweza kuwawezesha wananchi wa maeneo ya vijijini kufika sehemu ambazo zilikuwa hazifikiki kutokana na ujenzi unaoendelea wa barabara na madaraja katika maeneo mbalimbali nchini kwa kutumia teknolojia mbadala zenye gharama nafuu.

Pia wakala huo umewawezesha wakulima kusafirisha mazao yao kutoka vijijini hadi maeneo ya masoko na kwenye maghala ikiwa ni katika jitihada za kupunguzia gharama mkulima.

Akizungumza Agosti 4,2024 kwenye Maonesho ya Wakulima na Wafugaji Nanenane ambayo kitaifa yanafanyika jijini Dodoma, Mratibu wa Madaraja na Barabara za Mawe kutoka Tarura, Mhandisi Mshauri, Phares Ngeleja, ameeleza kuwa ili kuwafikia wananchi kwa haraka wanajenga barabara kwa kutumia mawe ambapo katika Mkoa wa Mwanza wamejenga kilomita 20 za mawe, Kigoma (kilomita 3.34), Rukwa (mita 350), Morogoro (mita 310).

Mhandisi Ngeleja amesema mesema wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali ambazo zimewezesha ujenzi wa madaraja na barabara na kwamba tangu wakala huo ulipoanzishwa mwaka 2017 wamejenga madaraja 275 nchi nzima yaliyogharimu Sh bilioni 10 huku Mkoa wa Kigoma ukiwa unaongoza na kwamba kama wangejenga kwa kutumia zege na nondo wangetumia zaidi ya Sh bilioni 50.

Ameongeza kuwa wanatumia teknolojia zingine huku akitolewa mfano katika Mkoa wa Dodoma wana barabara ya daraja dogo kilomita moja, Chamwino zaidi ya kilomita saba, Iringa napo zaidi ya kilomita sita pamoja na Mkoa wa Simiyu.

" Tutatumia teknolojia hizi kufungua barabara nyingi zaidi tuwawezeshe wakulima wafike maeneo yasiyofikika na kuyafikia masoko kirahisi,” amesema Mhandisi Ngeleja.

Kaimu Meneja wa TARURA Jiji la Dodoma, Mhandisi Kasongo Morijo, amesema wana miradi ya matengenezo na miradi mikubwa ya lami ambayo inalenga kuhakikisha maeneo yanafikika kuwezesha upatikanaji huduma za kijamii na kutolea mfano ujenzi wa Barabara ya Kisima cha Nyoka – Nkuhungu kuhakikisha wananchi wanafika mjini bila kikwazo.

Ameongeza kuwa wanahudumia kilomita 1,189 za barabara na kati ya hizo 224 ni za changarawe, 715 za udongo na 248 za lami na kwamba wanataka kuhakikisha hadi mwaka 2025 maeneo mengi ya Jiji hilo yawe na lami na yaweze kupitika kwa wakati.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano TARURA, Catherine Sungura, ameeleza kuwa maonesho hayo wanayatumia kuelimisha Umma jinsi wanavyojenga miundombinu ya barabara, madaraja na mifereji.

“Kazi kubwa imefanyika nchini, vijijini tumefanya kazi kubwa ya kufungua barabara ambazo zimewasaidia wananchi kuinuka kiuchumi na kupata maendeleo. Barabara ambazo tunajenga zimewasaidia wananchi mfano wajawazito walikuwa wanapata shida kufika kwenye huduma za afya lakini hivi sasa wanapata huduma bila changamoto, watoto wanakwenda shule na wakulima wanasafirisha mazao yao,” amesema Sungura.

Aidha amesema wana miradi katika mashamba ya Chai Kilolo mkoani Iringa na Tukuyu mkoani Mbeya ambako kuna barabara za lami zinazowarahisishia wakulima kusafirisha chai na kwenda kiwandani.

“Kufunguliwa kwa barabara hizi kumewezesha uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na wa eneo husika kubadilika na tunaingiza kipato kwa serikali, tunajivunia kazi kubwa ambayo tumeifanya. Bado tuna vipaumbele vya kuhakikisha tunafika kusikofikika…tunawakaribisha wananchi wafike katika banda letu waone kazi kubwa inayofanywa na Tarura,” amesema Sungura.

Wakala huo umekasimiwa kusimamia kilomita 144,429.77 ambapo kazi kubwa inayofanywa ni ujenzi na ukarabati wa miundombinu hiyo.

Post a Comment

0 Comments

 KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UTAWALA, KATIBA NA SHERIA YANOLEWA