Na Asha Mwakyonde,DODOMA
TAASISI ya Chakula na Lishe Tanzania(TFNC), imesema kuwa muda si mrefu wasagishaji wote wakubwa wa lishe nchini watatakiwa kuongeza virutubishi kwenye vyakula ambapo tayari kanuni zimeshaandaliwa kwa ajili ya kuongeza virutubishi hivyo.
Virutubishi hivyo ni vitamini B12 'Folic acid' ambavyo vitawekwa kwenye unga wa ngano na mahindi wanaweka madini chuma na zinki 'zinc' ambapo mafuta ya kula wanaweka vitamini A na chumvi huongezwa madini joto.
Akizungumza leo Agosti 7, 2024 kwenye maonesho ya wakulima na Wafugaji Nane nane ambayo yanaendelea katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma Afisa Utafiti kutoka Taasisi hiyo Francis Millinga amesema kuwa Sheria imeshaandaliwa ambapo tayari wameshatengeneza kanuni kwa wazalishaji huku akisema kiwanda kimeshafunguliwa Mikocheni jijini Dar es Salaam cha kutengeneza virutubishi hivyo.
Ameeleza kuwa katika Taasisi hiyo wanaprogramu uogezeji virutubishi kwenye chakula ambapo kwa kushirikiana na wadau wengine Tanzania wakiwamo Shirika la Viwango Tanzania (TBS),Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI) ,ambayo inamilika maafisa lishe na afya na kwamba wanashirikiana nao kwenda kukagua sampuli kama zimeongezwa virutubishi hivyo.
Ameongeza kuwa Taasisi hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo pamoja na Shirika la Viwango Tanzania (TBS),wanahakikisha kila mwenye mashine kuweka na kinyunyuzi cha virutubishi.
"Kanuni imeshapitishwa wasagishaji wote na wengine hawa wadogo kanuni imeshapita itaanza kusimamiwa hivyo waongeze virutubishi kwenye chakula lengo ni kuondokana na vifo vya akina mama wenye umri wa uzazi miaka 15 hadi 49 ambao mara nyingi huwa wanapoteza maisha kwa kukosa damu," ameeleza.
"Tumekuja kushiriki maonesho haya kipekee kabisa tumekuja kutangaza maabara yetu kwa kutumia maabara hii tunafanya vipimo mbalimbali ikiwa ni pamoja na tafiti zenye ushahidi kwa kuangalia viashiria lishe na virutubishi ," ameeleza
Millinga amesema watanzania wamekuwa na dhana potofu huku akisema kwenye kazi zao ambazo wanaziratibu kuongeza virutubishi kuna baadhi wanawakwamisha ambapo husema virutubishi hivyo vina madhara.
Afisa Utafiti huyo amesema kutokana na hali hiyo wanawakwamisha kufanya kazi ambapo vifo vya akina mama vitaongezeka huku akisema virutubishi hivyo vimethibitishwa na TBS na kila kinachoingia kinachukuliwa na kinapimwa.
Akizungumzia udumavu wa watoto amesema kuna udumavu wa akili matezi shingo maarufu kama goita huku akisema wanawaambia wasagishaji wa chumvi waongeze madini joto ambayo yanasaidia wasiweze kupata matatizo hayo.
Millinga ameongeza kuwa mambo ya uoni hafifu na kinga ya mwili huwa wanawaambia wasagishaji waweke vitamini A kwenye mafuta ya kula huku akisema wana maabara huku akisema wakishawashauri wanachukua sampuli kuona kama wanafanya uongezeji wa virutubishi.
Amesema kuwa baada hapo huwa wanawafuatilia watumiaji kwa kufanya tafiti na kufuata yale makundi ambayo yapo kwenye athari ya kuathirika na masuala ya lishe.
Amefafanua kuwa Taasisi hiyo ina ratibu mambo ya uchafuzi wa chakula kwa kuwa yanaweza kusababisha vifo na kwamba kwa kushirikiana na Wizara ya kilimo wanawashauri watu kufuata kanuni bora za kilimo, uzalishaji na uhifadhi.
0 Comments