RC SENYAMULE ATANGAZA KAMPENI YA MSAADA WA KISHERIA KUWAFIKIA MAELFU DODOMA

Na Asha Mwakyonde, DODOMA

SERIKALI imeendelea kusogeza huduma za haki karibu zaidi na wananchi, baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule kutangaza kuanza kwa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia Awamu ya Pili, itakayofanyika mkoani hapa kuanzia Mei 1 hadi 15, 2026, ikiwa ni mwendelezo wa juhudi za kuhakikisha kila mwananchi anapata haki kwa urahisi na bila gharama.

Kauli mbiu ya kampeni hiyo ni, “Msaada wa Kisheria kwa Haki, Usawa, Amani na Maendeleo”, ikilenga kuakisi dira ya taifa ya kujenga jamii yenye haki na ustawi kwa wote ifikapo mwaka 2050.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 30,2026 jijini hapa Senyamule amesema kampeni hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa azma ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha upatikanaji wa haki, hususan kwa makundi yenye uhitaji zaidi wakiwemo wanawake, watoto, wazee, watu wenye ulemavu na vijana.

Amesema uzoefu wa utekelezaji wa awamu ya kwanza mwaka 2023 unaonesha mafanikio makubwa, ambapo jumla ya wananchi 86,947 walifikiwa na kupatiwa huduma za msaada wa kisheria, wakiwemo wanaume 42,298 na wanawake 44,649.

Aidha, amebainisha kuwa katika migogoro 818 iliyopokelewa, migogoro 452 ilitatuliwa huku mingine 366 ikiendelea kufanyiwa kazi, hali inayoonesha umuhimu wa kuendeleza kampeni hiyo ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.

Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Mkoa, katika awamu hii huduma zitakazotolewa bila malipo ni pamoja na ushauri wa kisheria, elimu ya sheria, uandaaji wa nyaraka za kisheria, uwakilishi mahakamani na katika mabaraza, utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala pamoja na huduma za usajili wa vyeti vya kuzaliwa na vifo kupitia Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA).

Ameongeza kuwa elimu kwa jamii itatolewa katika ngazi zote kuanzia wilaya, kata hadi mitaa na vijiji, sambamba na kufanyika katika maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya wananchi kama masoko, vituo vya mabasi na taasisi za elimu.

Senyamule ametaja baadhi ya vituo vitakavyotumika kutoa huduma hizo kuwa ni Uwanja wa Mtekelezo jijini Dodoma, Buigiri na Mlowa Barabarani (Chamwino), Kibaigwa na Mkoka (Kongwa), Mpwapwa Mjini na Kibakwe (Mpwapwa), Bahi Mjini, Chemba, Stendi ya Zamani Kondoa Mji pamoja na Pahi Senta katika Wilaya ya Kondoa.

Amewasihi wananchi wa Mkoa wa Dodoma kujitokeza kwa wingi kutumia fursa hiyo ili kupata huduma za msaada wa kisheria bila malipo, akisisitiza kuwa haki ni msingi wa ustawi wa jamii na kila mtu anapaswa kuilindwa.

Post a Comment

0 Comments

WANANCHI DODOMA WAITIKIA AWAMU  YA PILI  YA SAMIA LEGAL AID CAMPAIGN