Na Asha Mwakyonde, DODOMA
SEKTA ya nishati nchini inaendelea kushika nafasi ya kimkakati katika kukuza uchumi na ustawi wa jamii, huku Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) ikiimarisha usimamizi wake ili kuhakikisha huduma zinapatikana kwa ubora, usalama na ufanisi.
EWURA imeendelea kujidhihirisha kama mhimili mkuu wa uthabiti wa sekta ya nishati nchini, kufuatia utekelezaji wa majukumu yake ya kiudhibiti kwa ufanisi na weledi.
Katika kipindi ambacho Tanzania inaendelea kujijengea msingi imara wa uchumi wa viwanda na huduma, Mamlaka hiyo imekuwa kuwa ni mhimili muhimu wa kuhakikisha sekta ya nishati inakua kwa usalama, ubora na tija kwa wananchi.
Akiwasilisha bungeni hivi karibuni Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati Waziri wa Nishati kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Waziri wa Nishati Deogratius Ndejembi anasema hatua hiyo inaakisi namna juhudi za Serikali zilivyoleta matokeo chanya kuanzia Julai 2025 hadi Machi 2026, zikiwemo kuimarika kwa ubora wa huduma, ongezeko la uwekezaji na upanuzi wa miundombinu ya mafuta na gesi asilia nchini.
Anasema kuanzia Julai 2025 hadi Machi 2026, Serikali kupitia EWURA imeonyesha uthabiti wa kiudhibiti kwa kusimamia kwa karibu miundombinu, ubora wa huduma na kuvutia uwekezaji, huku mahitaji ya nishati yakiongezeka sambamba na kasi ya shughuli za kiuchumi nchini.
Waziri huyo anasema EWURA imeendelea kusimamia kwa ufanisi shughuli za mkondo wa kati na chini wa gesi asilia, ambapo jumla ya kaguzi 68 zilifanyika katika miundombinu ya uchakataji, usafirishaji na usambazaji katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani na Dar es Salaam.
Miundombinu hii, ikiwemo vituo vya gesi asilia iliyoshindiliwa (CNG), na mabomba ya gesi, ilibainika kukidhi viwango vya ubora vinavyotakiwa," anaeleza Waziri Ndejembi.
MATUMIZI YA GESI ASILIA
Katika kuimarisha matumizi ya gesi asilia, anafafanua kuwa EWURA ilitoa vibali tisa vya ujenzi wa vituo vya CNG, huku Dar es Salaam pekee ikipata vibali saba katika maeneo mbalimbali ikiwemo Mbezi Beach, Mbagala na Kigamboni.
Anaeleza kuwa hatua hiyo inaendana na juhudi za Serikali za kupanua matumizi ya nishati safi na rafiki kwa mazingira, hasa katika sekta ya usafirishaji.
Aidha, Waziri huyo anasema vibali saba vya ujenzi wa mabomba ya kusafirisha na kuunganisha gesi asilia vilitolewa kwa kampuni binafsi na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), hatua inayochochea upatikanaji wa nishati hiyo katika viwanda, taasisi na matumizi ya majumbani.
Kwa mujibu wa waziri Ndejembi leseni 17 zilitolewa kwa shughuli mbalimbali za gesi, zikionyesha kuongezeka kwa ushiriki wa sekta binafsi katika mnyororo wa thamani wa nishati.
Anaongeza kuwa katika sekta ndogo ya mafuta ya petroli, EWURA ilitoa leseni 636 za biashara pamoja na vibali 288 vya ujenzi wa miundombinu ya mafuta, ambapo sehemu kubwa ilielekezwa katika maeneo ya vijijini ili kupanua huduma.
"Ukaguzi wa ubora wa mafuta ulionyesha kuwa asilimia 93.83 ya sampuli zilizopimwa zilikidhi viwango, huku vituo vilivyokiuka taratibu vikichukuliwa hatua kali za kisheria," anasema.
Anabainisha kuwa Serikali iliendelea kutekeleza programu ya uwekaji vinasaba katika mafuta, ambapo zaidi ya lita bilioni 3.5 za petroli na dizeli ziliwekewa alama maalum kudhibiti ubora na mapato ya Serikali.
Waziri huyo anasema ukaguzi uliofanyika katika vituo 672 ulibaini baadhi ya ukiukwaji ambapo hatua zilizochukuliwa zikiwemo kufungia vituo na kuwachukulia hatua za kisheria wahusika.
Anaeleza kuwa ukaguzi huo unaonesha ongezeko la matumizi ya mafuta nchini, ambapo petroli ilifikia wastani wa lita milioni 6.28 kwa siku na dizeli lita milioni 8.42, ikichochewa na ukuaji wa sekta za uzalishaji, ujenzi na usafirishaji.
Hata hivyo, anafafanua kuwa matumizi ya mafuta ya taa yamepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na upanuzi wa huduma za umeme na matumizi ya nishati mbadala.
BEI ZA MAFUTA
Akizungumzia bei za mafuta anasema EWURA iliendelea kudhibiti bei za mafuta nchini kwa kuzingatia mwenendo wa soko la dunia.
"Licha ya kushuka kwa bei katika miezi ya awali, hali ya vita Mashariki ya Kati ilisababisha kupanda kwa bei kuanzia Januari 2026. Hata hivyo, kwa ujumla, bei za mafuta nchini zilibaki katika viwango vinavyoweza kumudu kwa wananchi ikilinganishwa na mwaka uliopita," anasema.
SEKTA YA UMEME
Anasema EWURA ilitoa leseni kwa kampuni mbalimbali kuzalisha umeme pamoja na kuidhinisha mikataba kati ya TANESCO na wazalishaji binafsi, hatua inayotarajiwa kuongeza zaidi ya megawati 98 katika gridi ya taifa.
Waziri Ndejembi anabainisha kuwa zaidi ya mafundi umeme 1,000 walipatiwa leseni, jambo linaloimarisha usalama wa mifumo ya umeme nchini.
"Hatua hizi zinaonesha dhamira ya Serikali ya kuendelea kuimarisha udhibiti wa sekta ya nishati ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora, salama na endelevu," anasema.
Serikali imeeleza kuwa itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na mifumo ya kidijitali ili kuongeza ufanisi katika usimamizi wa mafuta na gesi asilia, huku ikitoa wito kwa sekta binafsi kuchangamkia fursa zilizopo katika sekta hiyo muhimu kwa maendeleo ya Taifa.
.jpeg)
0 Comments