Na Asha Mwakyonde, DODOMA
SERIKALI imeeleza mpango mpana wa kuimarisha na kuongeza fursa za elimu ya juu nchini kwa mwaka wa fedha 2026/2027, ikilenga kuongeza idadi ya wanafunzi, kuimarisha ubora wa mafunzo pamoja na kuhakikisha vijana wengi zaidi wananufaika na mikopo na ufadhili wa masomo katika nyanja mbalimbali za kitaaluma.
Hayo yamesemwa leo Mei 7,2026 bungeni jijini hapa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda wakati akiwasilisha Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027 amesema serikali imejipanga kuratibu udahili wa wanafunzi takribani 180,000 watakaojiunga na masomo ya shahada ya kwanza katika vyuo mbalimbali vya elimu ya juu nchini.
Amesema sambamba na hatua hiyo, serikali itaongeza idadi ya wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu kutoka wanafunzi 252,773 mwaka 2025/2026 hadi 292,981 mwaka 2026/2027 ili kuhakikisha fursa za elimu hazikwami kutokana na changamoto za kifedha.
Aidha, Prof. Mkenda amesema serikali itaendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi 24,978 wa stashahada katika fani za sayansi na ufundi, hatua inayolenga kuongeza wataalamu wenye ujuzi unaohitajika katika uchumi wa viwanda.
Prof. Mkenda ameeleza kuwa katika kuimarisha masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM), serikali itaongeza idadi ya wanufaika wa SAMIA Scholarship kutoka wanafunzi 2,630 hadi 2,738 katika mwaka wa fedha 2026/2027.
"Kupitia programu ya Samia Extended Scholarship DS/AI+, serikali pia itaongeza wanafunzi kutoka 50 hadi 100 watakaopelekwa kusoma nje ya nchi katika fani za sayansi data, sayansi shirikishi na akili unde (AI)," amesema.
Prof. Mkenda amesema hatua hiyo inalenga kuandaa wataalamu wa kisasa watakaoweza kushindana katika soko la ajira la kimataifa na kuchochea maendeleo ya sayansi na teknolojia nchini.
Ameeleza kuwa katika kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, serikali itaendelea kutoa ufadhili kwa wanafunzi wa kigeni wanaosoma Kiswahili nchini Tanzania, ambapo wanafunzi 15 kutoka China, wawili kutoka Oman na watano kutoka Hungary wataendelea kunufaika na programu hiyo.
Amesema hatua hiyo inalenga kukuza na kueneza lugha ya Kiswahili duniani pamoja na kuimarisha diplomasia ya elimu.
Akizungumzia kuhusu miundombinu, Prof. Mkenda amesema serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika taasisi 21 za elimu ya juu kupitia ujenzi na ukarabati wa vyumba vya mihadhara, madarasa, maabara, maktaba na ofisi.
Aidha, ameongeza kuwa serikali itaendelea kuimarisha ubora wa elimu ya juu kwa kufanya ithibati ya programu 300 za masomo na kukagua vyuo vikuu 25 nchini ili kuhakikisha viwango vya elimu vinazingatia ubora, miundombinu na uendeshaji bora.
Amesisitiza kuwa hatua hizo ni sehemu ya mkakati wa taifa wa kuhakikisha elimu ya juu inazalisha wataalamu wabunifu na wenye uwezo wa kuchangia maendeleo ya uchumi wa viwanda.


0 Comments