NBS YABAINISHA CHANGAMOTO ZA UWEZESHAJI WANAWAKE KIUCHUMI NA KIJAMII

Na Mwakyonde,DODOMA

SERIKALI imeeleza kuwa itaendelea kuimarisha jitihada za kuwawezesha wanawake kijamii na kiuchumi pamoja na kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia, hii ni baada ya tafiti mpya zilizofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kubaini kuwa wanawake wengi bado hawana uhuru wa kutosha katika kufanya maamuzi muhimu yanayohusu maisha yao, uchumi na ustawi wa familia.

Hali hiyo imebainika kupitia ripoti mbili mpya zilizozinduliwa juzi jijini Dodoma ambazo ni Utafiti wa Mazingira na Jinsia 2025 pamoja na Utafiti wa Uwezeshaji Wanawake na Lishe 2023/2024, ambapo matokeo yake yameonesha changamoto mbalimbali zinazoendelea kuwakabili wanawake nchini katika maeneo ya kiuchumi, kijamii, lishe na mabadiliko ya tabianchi.

Akizindua ripoti hizo, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk.Dorothy Gwajima alisema tafiti hizo zimefungua ukurasa mpya wa uelewa kuhusu hali halisi ya wanawake nchini na namna mazingira yanavyoathiri maendeleo yao.

Alisema matokeo ya tafiti hizo yanaonesha kuwa ni asilimia 26 pekee ya wanawake wanaoamini kuwa mwanamke anapaswa kuwa na uhuru wa kufanya maamuzi kuhusu shughuli zake za kiuchumi, hali inayodhihirisha kuwa bado wanawake wengi hawajajengewa mazingira ya kujiamini na kushiriki kikamilifu katika masuala ya maendeleo.

“Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha wanawake wanapata sauti, haki na nafasi ya kufanya maamuzi yanayogusa maisha yao. Kupambana na ukatili wa kijinsia ni sehemu muhimu ya safari hiyo,” alisema Dk. Gwajima.

Alifafanua kuwa kiwango hicho ni kikubwa zaidi Zanzibar ambapo asilimia 44.9 ya wanawake wanaamini katika uhuru huo wa kiuchumi ikilinganishwa na Tanzania Bara yenye asilimia 23 pekee.

Kwa upande wa maamuzi kuhusu ndoa, talaka na uzazi, utafiti umeonesha kuwa asilimia 34.1 ya wanawake wanaunga mkono uhuru wa mwanamke kufanya maamuzi hayo, huku Kanda ya Kusini ikiongoza kwa asilimia 70.2 ikifuatiwa na Kanda ya Mashariki kwa asilimia 57.4.

Aidha, alifafanua kuwa zaidi ya nusu ya wanawake nchini sawa na asilimia 54.6 wameonesha kutokubaliana na aina zote za ukatili wa kijinsia, ambapo Zanzibar imeongoza kwa asilimia 74.9 dhidi ya asilimia 53.7 ya Tanzania Bara.

Dk. Gwajima aliongeza kuwa ripoti hiyo pia imebainisha tofauti katika uwezo wa kufanya maamuzi ndani ya kaya, ambapo wanawake wameonekana kuwa na ushawishi mkubwa zaidi katika matumizi ya muda kwa asilimia 43.3 ikilinganishwa na wanaume wenye asilimia 39.4.

"Hata hivyo, wanaume bado wanaendelea kuongoza katika maamuzi ya matumizi ya fedha kwa asilimia 54.8 huku wanawake wakiwa na asilimia 39.6 pekee.

Pamoja na wanawake kuwa na uhuru mkubwa zaidi katika kupanga matumizi ya muda na maamuzi ya afya binafsi, bado wako nyuma katika maamuzi ya matumizi ya fedha ukilinganisha na wanaume,” alisema.

Katika eneo la rasilimali na huduma za kifedha, utafiti umeonesha kuwa asilimia 58 ya wanawake wanatumia huduma za kifedha ikilinganishwa na asilimia 72 ya wanaume, huku asilimia 40 pekee ya wanawake wakimiliki mali na ni theluthi moja tu kati yao wenye hati rasmi za umiliki.

Akizungumzia lishe, alieleza kuwa tafiti zimebaini kuwa asilimia 56.7 ya wanawake wanakidhi kiwango cha chini cha lishe bora, huku hali ikiwa nzuri zaidi maeneo ya mijini kuliko vijijini ambako wanawake wengi bado wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa lishe bora.

Alisema, matumizi ya vyakula vya asili ya wanyama kama mayai na matunda yameonekana kuwa chini zaidi katika maeneo ya vijijini, jambo linaloathiri afya na ustawi wa familia nyingi.

Dk. Gwajima alisema tafiti hizo pia zimeonesha kuwa mwanamke aliyewezeshwa kiuchumi na kijamii huwa na uwezo mkubwa zaidi wa kuboresha lishe yake binafsi pamoja na ya familia yake kwa ujumla.

Waziri huyo alisema katika eneo la mazingira, matokeo ya Utafiti wa Mazingira na Jinsia yameonesha kuwa wanawake na wanaume wote wameendelea kuathiriwa kwa kiwango kikubwa na mabadiliko ya tabianchi, hususan katika maeneo ya vijijini na nyanda kame.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, asilimia 82.9 ya wanawake na asilimia 80.8 ya wanaume Tanzania Bara wamekumbwa na angalau athari moja ya mabadiliko ya tabianchi, huku ukame ukiendelea kuwa tatizo kubwa zaidi katika maeneo mengi ya vijijini.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk. Amina Msengwa alisema NBS itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuzalisha tafiti zenye tija kwa maendeleo ya taifa na ustawi wa wananchi.

Alisema tafiti hizo zitasaidia serikali, wataalamu na wadau kupanga sera na mikakati sahihi ya kuwawezesha wanawake, kuboresha lishe na kukabiliana na changamoto za mazingira nchini

Post a Comment

0 Comments

WATOTO WENYE ULEMAVU WANAHITAJI SHULE JUMUISHI KILA MKOA