Na Asha Mwakyonde,DODOMA
SEKTA ya elimu nchini inaendelea kushuhudia mageuzi makubwa yanayolenga kuongeza fursa za masomo, kuboresha ubora wa ufundishaji na kuhakikisha wahitimu wanapata ujuzi unaohitajika katika soko la ajira la sasa na la baadaye. Maboresho hayo yamejikita pia katika kuimarisha matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu kama msingi muhimu wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Hayo yameelezwa leo Mei 7,2026 na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda alipowasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/2026 bungeni, ambapo amebainisha kuwa serikali imejielekeza katika vipaumbele vitano vikuu vinavyolenga kujenga rasilimaliwatu yenye ujuzi na ushindani wa kimataifa.
Amevitaja vipaumbele hivyo kuwa ni kuendelea na utekelezaji wa sera na mitaala pamoja na mapitio ya sheria za elimu, kuimarisha mafunzo ya amali katika shule za sekondari na vyuo vya ufundi stadi, kuongeza ubora wa elimu ya awali, msingi, sekondari na ualimu, kuimarisha elimu ya juu pamoja na kuendeleza utafiti na ubunifu katika sayansi na teknolojia.
Prof. Mkenda amesema vipaumbele hivyo vimechaguliwa kwa kuzingatia mahitaji ya uchumi wa viwanda, kuongeza fursa za ajira kwa vijana na kuimarisha ushindani wa taifa katika soko la kimataifa.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo amesema serikali inaendelea na maandalizi ya utekelezaji wa sera ya elimu ya lazima ya miaka 10, ambapo takribani wanafunzi 3,021,177 wanatarajiwa kujiunga na elimu ya sekondari kidato cha kwanza ifikapo Januari 2028.
Amefafanua kuwa mpango huo unalenga kuhakikisha mwanafunzi anakaa ndani ya mfumo wa elimu kwa muda wa kutosha hadi kufikia umri wa kujiajiri au kuajiriwa, ambapo mabadiliko hayo yatamwezesha kijana kumaliza elimu ya lazima akiwa na takribani miaka 16.
“Lengo ni kuhakikisha hakuna kijana anayetoka kwenye mfumo wa elimu kabla ya kuwa na ujuzi unaomwezesha kujiajiri au kuajiriwa,” amesema Prof. Mkenda.
Ameongeza kuwa serikali pia imeendelea na ujenzi wa miundombinu ya elimu ikiwemo madarasa, maabara, karakana pamoja na ajira za walimu kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI ili kujiandaa na ongezeko la wanafunzi.
Katika kuhakikisha mfumo wa elimu unakuwa wa kisasa zaidi, Waziri huyo amesema serikali imeendelea kufanya mapitio ya Sheria ya Elimu Sura ya 353 ambapo tayari maoni ya wadau yamekusanywa na taarifa ya awali ya mapitio kuandaliwa.
Aidha, amesema serikali imeandaa viunzi na miongozo mbalimbali ikiwemo Kiunzi cha Umahiri wa Walimu katika TEHAMA 2026 pamoja na mwongozo wa ushirikiano kati ya serikali na wadau wa teknolojia za kidijitali katika sekta ya elimu.
Katika eneo la elimu jumuishi, Prof. Mkenda alisema serikali imeandaa miongozo nane muhimu ikiwemo matumizi ya TEHAMA kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum, lugha ya alama ya Tanzania, pamoja na elimu ya amali kwa wanafunzi hao ili kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma.
Amebainisha pia kuwa ndani ya siku 100 za uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, serikali imeanzisha Mpango Mkakati wa Kisayansi wa Kujenga Umahiri wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa watoto wa elimu ya awali na darasa la kwanza na la pili, unaolenga kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayefika darasa la tatu bila kumudu stadi hizo muhimu.
Aidha, amesema serikali imezindua mpango wa ushirikiano kati ya waajiri, vyuo vya ufundi stadi na vyuo vikuu, unaolenga kuimarisha mafunzo kwa vitendo na kupunguza changamoto ya kutokuwepo uwiano kati ya ujuzi wa wahitimu na mahitaji ya soko la ajira.
Prof. Mkenda amesisitiza kuwa mpango huo utasaidia kuongeza ajira kwa wahitimu, kuimarisha mafunzo ya vitendo na kuhakikisha elimu inazalisha wataalamu wanaokidhi mahitaji ya viwanda na uchumi wa kisasa.




0 Comments