BRELA YAANDIKA HISTORIA YA MIAKA SABA YA UAMINIFU KWA SERIKALI


Na Asha Mwakyonde DAR ES SALAAM 

WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umeendelea kudhihirisha uimara wake katika usimamizi wa rasilimali za umma baada ya kutunukiwa tuzo ya nafasi ya tatu miongoni mwa taasisi zinazowasilisha gawio kwa Serikali kwa wakati na kwa uendelevu, mafanikio yaliyodumu kwa miaka saba mfululizo.

Tuzo hiyo imetolewa Juni 30, 2026, katika hafla ya utoaji wa gawio kwa Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/2026 iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam, mbele ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza katika hafla hiyo, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, amesema BRELA ni miongoni mwa taasisi zilizoonyesha mfano wa kuigwa kwa kuwasilisha gawio kwa wakati, kwa uthabiti na kwa kuzingatia matakwa ya sheria kwa kipindi chote cha miaka saba.

Amesema taasisi zilizotunukiwa katika kundi hilo zimeendelea kutekeleza wajibu wao kwa ufanisi huku zikichangia mapato ya Serikali kwa kiwango kinachostahili.

"Katika kundi hili tumezingatia taasisi zinazochangia gawio kwa wakati na kwa uendelevu. BRELA imeendelea kufanya hivyo kwa uthabiti na kwa kipindi cha miaka saba imekuwa ikichangia wastani wa Sh bilioni 15.6 kila mwaka," ameleza Mchechu.

Tuzo hiyo ilipokelewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara kwa BRELA, Prof. Neema Mori, akiwa ameambatana na Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa.

Baada ya kupokea tuzo hiyo, Nyaisa amewapongeza watumishi wa BRELA kwa juhudi na kujituma kwao, akisema mafanikio hayo ni matokeo ya utendaji wenye nidhamu, weledi na uwajibikaji.

Amesisitiza kuwa tuzo hiyo ni ya watumishi wote wa BRELA na kuwataka kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili taasisi iendelee kuwa mfano katika utoaji wa huduma na kuchangia maendeleo ya taifa.

"Hii ni tuzo ya watumishi wote wa BRELA. Nawapongeza kwa kazi nzuri mnayoifanya. Mafanikio haya ni matokeo ya juhudi zenu, na nina imani mtaendelea kufanya kazi kwa bidii zaidi ili kupata mafanikio makubwa zaidi," amesema Nyaisa.

Katika hafla hiyo, BRELA pia ilikabidhi Serikali gawio la Sh bilioni 11.49, ikiwa ni sehemu ya mchango wake katika kuongeza mapato ya Serikali na kuunga mkono utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo nchini.

Post a Comment

0 Comments

CFR YATAKA VIJANA KUTUMIA FURSA ZA DIPLOMASIA YA UCHUMI