Na Asha Mwakyonde, DODOMA
SERIKALI imesema utekelezaji wa miradi ya maendeleo unaendelea kuzaa matunda makubwa katika sekta mbalimbali huku uchumi wa Taifa ukiendelea kuimarika, ikieleza kuwa mafanikio hayo yanatokana na uwekezaji wa kimkakati unaolenga kuboresha maisha ya wananchi na kujenga uchumi unaojitegemea.
Hayo ameyasema leo Juni 28,2026 jijini hapa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwa wananchi, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imeendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo katika sekta za nishati, kilimo, miundombinu, usafiri, afya, elimu na huduma nyingine za kijamii, hatua ambazo zimechangia kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi na kuboresha huduma kwa wananchi.
Amesema uchumi wa Tanzania uliendelea kukua kwa asilimia 5.9 mwaka 2025 na unatarajiwa kufikia asilimia 6.3 mwaka 2026, huku mfumuko wa bei ukiendelea kubaki ndani ya kiwango kinachokubalika cha asilimia 3.4.
Aidha, amesema bajeti ya Serikali ya mwaka 2026/27 ya Shilingi trilioni 62.33 imeongeza uwezo wa nchi kujitegemea, ambapo asilimia 74.2 ya bajeti hiyo itagharamiwa na mapato ya ndani, hatua aliyoitaja kuwa mafanikio makubwa katika kujenga uchumi wa kujitegemea.
Akizungumzia ushirikiano wa kimataifa, Msigwa amesema ziara ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan nchini Urusi imefungua fursa mpya za uwekezaji na biashara katika sekta za nishati ya uranium, kilimo, usafiri wa anga, utalii, elimu na teknolojia.
Msemaji huyo amebainisha kuwa makubaliano yaliyofikiwa pia yatawezesha kuanza kwa safari za moja kwa moja za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL),kati ya Dar es Salaam, Zanzibar na Moscow pamoja na kuongezeka kwa nafasi za ufadhili wa masomo kwa Watanzania nchini Urusi.
Msigwa amesema Serikali imeendelea kutumia mikopo kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo yenye tija, ikisisitiza kuwa tathmini mbalimbali zinaonesha deni la Taifa bado ni himilivu na liko ndani ya viwango vinavyokubalika kimataifa.
Katika sekta ya nishati, amesema kukamilika kwa Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) pamoja na utekelezaji wa miradi mingine ya uzalishaji na usafirishaji wa umeme umeongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme nchini na kuimarisha upatikanaji wa huduma hiyo kwa wananchi na wawekezaji.
Msigwa ameeleza kuwa mageuzi yaliyofanyika katika sekta ya usafiri na uchukuzi yameongeza ufanisi katika Bandari ya Dar es Salaam, Shirika la Reli Tanzania (TRC) na Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), hatua zinazochangia kukuza biashara, usafirishaji na mapato ya Serikali.
Aidha, amewataka Watanzania kuendelea kulipa kodi na kushiriki katika shughuli za uzalishaji ili kuendelea kuimarisha uchumi wa Taifa, akisisitiza kuwa maendeleo ya Tanzania yanategemea juhudi za wananchi wake.
Katika hatua nyingine, Msigwa amewashukuru waandishi wa habari kwa kuendelea kuripoti shughuli za maendeleo kwa weledi na uzalendo, huku akiwataka kuendelea kuzingatia maadili ya taaluma na maslahi ya Taifa katika utekelezaji wa majukumu yao.




0 Comments