Na Asha Mwakyonde, DODOMA
KUPANDA kwa bei za mafuta duniani kukiendelea kuongeza gharama za usafiri na uzalishaji, Watanzania wametakiwa kuchangamkia matumizi ya gesi asilia kama mbadala nafuu wa nishati utakaosaidia kupunguza gharama za uendeshaji wa vyombo vya usafiri na shughuli nyingine za kiuchumi.
Wito huo umetolewa leo Juni 4,2026 katika maonesho ya wiki ya mazingira inayo kwenda sambamba kilele cha mazingira duniani na Afisa Mwandamizi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC),Eugene Isaya, alipozungumza na wananchi waliotembelea banda la shirika hilo, ambapo ameeleza faida mbalimbali za matumizi ya gesi asilia nchini.
Isaya amesema TPDC ni Shirika la Mafuta la Taifa lililo chini ya Wizara ya Nishati na lina jukumu la kusimamia na kuendeleza rasilimali za petroli na gesi asilia kwa manufaa ya Watanzania.
Amsema matumizi ya gesi asilia yanaendelea kuwa suluhisho muhimu kutokana na gharama zake kuwa nafuu ikilinganishwa na mafuta ya petroli, sambamba na kusaidia kupunguza gharama za matengenezo ya vyombo vya moto.
“Kwa mfano, gari hili tulilonalo hapa lina injini ya ukubwa wa CC 1300 na limefungwa mtungi wa kilogramu 11 Mtungi huo unaweza kujazwa gesi asilia kwa shilingi 17,000 tu, sawa na wastani wa shilingi 1,550 kwa kila kilogramu ya gesi,” amesema.
Amefafanua kuwa kiasi hicho cha gesi kina uwezo wa kuliwezesha gari kusafiri umbali wa kati ya kilomita 160 hadi 220, wakati kwa umbali huo huo mtumiaji wa petroli atalazimika kutumia kati ya lita 10 na 14 za mafuta.
Kwa mujibu wa Isaya, mlinganisho wa gharama unaonesha kuwa mtumiaji wa gesi asilia anaweza kutumia shilingi 17,000 kusafiri hadi kilomita 220, huku mtumiaji wa petroli akitumia zaidi ya shilingi 50,000 kwa umbali huo huo.
Aidha, ameongeza kuwa mzozo unaoendelea katika eneo la Mashariki ya Kati umechangia kupanda kwa bei za mafuta katika soko la dunia, hali inayofanya matumizi ya gesi asilia kuwa fursa muhimu zaidi kwa wananchi na wawekezaji.
Kutokana na hali hiyo,Isaya amewahamasisha wananchi pamoja na sekta binafsi kuwekeza katika huduma za ubadilishaji wa mifumo ya magari ili yaweze kutumia gesi asilia badala ya mafuta ya petroli.
Afisa huyo ametoa wito kwa wawekezaji wa sekta binafsi kuanzisha vituo vya kujaza gesi asilia kwa magari, akisema uwekezaji huo utasaidia kuongeza upatikanaji wa huduma hiyo kwa wananchi huku ukiwa chanzo cha faida kwa wawekezaji.
“Tunazialika kampuni na wawekezaji mbalimbali kuchangamkia fursa hii. Kadri vituo vya gesi asilia vitakavyoongezeka, ndivyo Watanzania wengi zaidi watakavyonufaika kwa kupunguza gharama za nishati na uchumi wa nchi kuendelea kukua,” amesema.

0 Comments