BRELA YAWAHIMIZA WAJASIRIAMALI KURASIMISHA BIASHARA, KULINDA ALAMA ZAO


Na Asha Mwakyonde, DAR ES SALAAM

WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umewataka wajasiriamali wanaoshiriki Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) kutumia fursa ya huduma zinazotolewa na wakala huo kwa kusajili biashara, majina ya biashara na alama za bidhaa ili kuendesha shughuli zao kwa mujibu wa sheria na kujikinga dhidi ya migogoro ya kisheria.

Rai hiyo imetolewa Julai 10, 2026 na Ofisa Usajili wa BRELA, Benedickson Wilson, alipokuwa akitoa mafunzo kuhusu umuhimu wa kurasimisha biashara kwa wajasiriamali wanawake katika banda la Chemba ya Wafanyabiashara Wanawake Tanzania (TWCC), na banda la Wafanyabiashara wa Mkoa wa Ruvuma kwenye Maonesho ya Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam.

Wilson amesema usajili wa biashara na alama za biashara ni hatua muhimu inayowapa wafanyabiashara ulinzi wa kisheria, huongeza uaminifu wa biashara zao na kuwawezesha kushindana kwa haki katika soko.

Akizungumzia Sheria ya Alama za Biashara na Huduma, amesema usajili wa alama humpa mmiliki haki ya kipekee ya kuitumia na kumkinga dhidi ya mtu mwingine anayeweza kuitumia bila idhini au kusajili alama inayofanana na kusababisha mkanganyiko kwa watumiaji.

"Usajili wa alama hufanyika kulingana na aina ya biashara, ambapo kuna madaraja 45 ya bidhaa na huduma. Kwa mfano, mfanyabiashara wa vipodozi atasajili alama yake katika Daraja la 3. Baada ya usajili, mmiliki hupata haki ya kipekee ya kuitumia na kumzuia mtu mwingine kuitumia bila ruhusa," amesema Wilson.

Ameongeza kuwa usajili wa alama za biashara husaidia kutofautisha bidhaa au huduma za mzalishaji mmoja na mwingine, jambo linaloimarisha ushindani wa haki na kuwalinda watumiaji dhidi ya mkanganyiko wanaponunua bidhaa au huduma sokoni.

Aidha, ameeleza kuwa mfanyabiashara aliyesajili alama yake ana haki ya kuchukua hatua za kisheria endapo mtu mwingine atatumia au atasajili alama inayofanana bila idhini, kwa mujibu wa Sheria ya Alama za Biashara na Huduma.

Kwa upande wao, baadhi ya wajasiriamali walioshiriki mafunzo hayo wamesema elimu waliyoipata imewaongezea uelewa kuhusu hatua za kurasimisha biashara, kusajili majina ya biashara pamoja na kulinda alama zinazotambulisha bidhaa na huduma zao.

"Nilikuwa sifahamu vizuri huduma zinazotolewa na BRELA, lakini kupitia mafunzo haya nimeelewa umuhimu wa kusajili jina la biashara na alama yangu. Pia nimefahamu kuwa usajili wa jina la biashara unaweza kukamilika ndani ya siku moja na kupata cheti cha usajili. Tunawashukuru sana BRELA kwa elimu hii," amesema Melania Shawa.

BRELA inaendelea kutoa elimu na huduma kwa washiriki wa Maonesho ya Sabasaba kupitia mabanda yake mawili; banda kuu lililopo karibu na Banda la Wizara ya Fedha na banda lililopo ndani ya Banda la Wizara ya Viwanda na Biashara.

Wananchi na washiriki wa maonesho wanahimizwa kutembelea mabanda hayo ili kupata elimu na huduma mbalimbali za usajili hadi siku ya kilele cha maonesho hayo, Julai 13, 2026.

Post a Comment

0 Comments

USULUHISHI WA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA WAOKOA MGOGORO WA KIBIASHARA