Na Asha Mwakyonde, DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imewahimiza Watanzania kuachana na matumizi ya nishati zisizo safi kama mkaa na kuni na badala yake kutumia nishati safi, ikieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kulinda mazingira, kuboresha afya za wananchi na kupunguza gharama za maisha kwa muda mrefu.
Akizungumza katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Meneja wa Uhusiano na Mawasiliano wa EWURA,David Mwakalosi, amesema matumizi ya nishati safi ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuhakikisha wananchi wanaishi katika mazingira salama na yenye afya.
Amesema matumizi ya mkaa na kuni yanasababisha ukataji mkubwa wa miti, jambo linalochochea uharibifu wa mazingira na kupunguza uwezo wa misitu kuhifadhi mfumo wa ikolojia pamoja na kusafisha hewa.
"Unapotumia mkaa au kuni, unachangia kukatwa kwa miti ambayo imechukua miaka mingi kukua. Hivyo, matumizi ya nishati safi yanasaidia kulinda mazingira na rasilimali za taifa," amesema.
Mwakalosi ameeleza kuwa pamoja na athari za kimazingira, matumizi ya mkaa hupoteza muda mwingi wa kuandaa moto kabla ya kuanza kupika, huku nishati kama gesi na umeme zikiruhusu mpishi kuanza kupika mara moja na kudhibiti kiwango cha joto kwa urahisi.
Ameongeza kuwa matumizi ya nishati safi huongeza ufanisi wa matumizi ya muda, huku wananchi wakipata nafasi ya kufanya shughuli nyingine za uzalishaji badala ya kutumia muda mwingi kuandaa mkaa.
Aidha, amesema wengi hudhani matumizi ya mkaa ni nafuu, lakini wakifanya hesabu za matumizi ya kila siku kwa mwezi au mwaka hugundua kuwa gharama zake ni kubwa kuliko matumizi ya nishati safi.
"Ni kweli kununua jiko la gesi au vifaa vya kutumia umeme kunaweza kuonekana ni gharama kubwa mwanzoni, lakini ni uwekezaji unaopunguza matumizi kwa muda mrefu na kuongeza urahisi wa maisha," amesema.
Akizungumzia kuhusu afya, Mwakalosi amesema moshi unaotokana na mkaa na kuni ni hatari kwa afya za watumiaji na unaweza kusababisha magonjwa ya mfumo wa upumuaji, huku wakati mwingine ukisababisha vifo kutokana na kuvuta hewa yenye sumu inayotokana na mwako usio kamili.
Ametolea mfano baadhi ya matukio yaliyowahi kuripotiwa katika mikoa yenye baridi, ambapo watu wamepoteza maisha baada ya kuwasha mkaa ndani ya nyumba kwa ajili ya kujipatia joto.
Amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan inaendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia, unaolenga kuhakikisha ifikapo mwaka 2034 angalau asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia.
Mwakalosi amefafanua kuwa nishati safi haimaanishi gesi na umeme pekee, bali pia matumizi ya majiko ya kisasa yenye teknolojia ya kuokoa nishati, yakiwemo majiko ya umeme yenye uwezo wa kupima kiwango cha umeme kinachotumika wakati wa kupika.
Ameongeza kuwa baadhi ya kampuni zinazoshiriki maoneshoni zimeanza kuuza majiko hayo kwa mfumo wa malipo ya awamu, hatua inayowawezesha wananchi wengi kuyamudu.
Amewataka wananchi kutembelea banda la EWURA katika Maonesho ya Sabasaba ili kupata elimu zaidi kuhusu matumizi ya nishati safi, pamoja na kufuatilia taarifa kupitia mitandao ya kijamii ya mamlaka hiyo ikiwemo Facebook, Instagram na YouTube.



0 Comments