📍Yahimiza mazungumzo kuokoa ndoa na kudumisha amani ya familia
Na Asha Mwakyonde, DAR ES SALAAM
KATIKA kipindi ambacho migogoro ya ndoa na familia inaendelea kuwa moja ya changamoto zinazoathiri ustawi wa jamii, Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria inaendelea kusisitiza umuhimu wa kutumia njia za utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala (Alternative Dispute Resolution - ADR),kama nyenzo ya kulinda taasisi ya ndoa, kuimarisha malezi ya watoto na kudumisha amani ya jamii.
Badala ya kukimbilia mahakamani, wananchi wanahimizwa kujenga utamaduni wa mazungumzo, maridhiano na usuluhishi ili kupata suluhisho la kudumu litakalowanufaisha wanandoa, watoto na Taifa kwa ujumla.
Akizungumza kwenye banda la Wizara hiyo katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), 'Sabasaba' Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Utatuzi wa Migogoro kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Wakili Felix Chakila anasema ushiriki wa Wizara katika maonesho hayo unalenga kuwapatia wananchi huduma mbalimbali zinazotolewa pamoja ikiwa ni pamoja na elimu ya sheria kuhusu masuala yanayogusa maisha yao ya kila siku.
Anasema elimu hiyo inahusisha maeneo mbalimbali ya sheria, ikiwemo sheria za mikataba, haki za wananchi na hasa umuhimu wa utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala, hususan migogoro ya ndoa na familia.
Kwa mujibu wa Chakila, Serikali inatambua kuwa ndoa ni msingi wa familia, na familia ndiyo nguzo ya amani, maendeleo na mshikamano wa jamii.
Anaeleza kuwa Wizara inatambua Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na kwamba inatambua ndoa kama nguzo muhimu katika amani na kuimarisha jamii iliyoimara.
Wakili Chakila ameeleza kuwa kutokana na umuhimu huo, Wizara inaendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria ya ndoa na kuhamasisha matumizi ya maridhiano na usuluhishi katika kushughulikia migogoro ya kifamilia.
Anasema utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala una manufaa makubwa kwa jamii kwani huimarisha amani na mshikamano ndani ya familia, hupunguza migogoro inayofikishwa mahakamani na kusaidia kupunguza ongezeko la talaka zisizo za lazima.
Aidha, anaeleza kuwa njia hiyo hujenga mazingira ya maelewano, hupunguza chuki na uhasama kati ya wanafamilia na kuchangia malezi bora ya watoto kwa kuhakikisha wanakulia katika mazingira yenye utulivu na ushirikiano wa wazazi.
Chakila anasema Wizara ina jukumu la kitaifa la kuwaelimisha wananchi kuhusu haki zao, wajibu wao na taratibu za kisheria zinazolenga kulinda taasisi ya ndoa ili familia ziendelee kuwa msingi imara wa maendeleo ya Taifa.
Anabainisha kuwa migogoro ya ndoa inapotokea, hatua ya kwanza inayoshauriwa ni kuipeleka kwenye vyombo vya usuluhishi vinavyotambulika kisheria badala ya kukimbilia mahakamani.
"Sheria ya ndoa, Sura ya 29 ya mwaka 1971 kama ilivyorekebishwa mwaka 2019 imeanzisha Mabaraza ya Usuluhishi wa ndoa katika ngazi ya kata, yenye jukumu la kupokea na kusikiliza migogoro ya wanandoa kabla ya hatua nyingine za kisheria kuchukuliwa," anasema
Mbali na mabaraza hayo, anasema taasisi za dini zimeendelea kutoa mchango mkubwa katika kusuluhisha migogoro ya ndoa kwa kuzingatia misingi ya dini, maadili na maridhiano kwa lengo la kuwapatanisha wanandoa na kurejesha amani katika familia.
Akielezea namna mchakato wa usuluhishi unavyofanyika, Chakila anasema huanza pale mmoja wa wanandoa anapowasilisha malalamiko kwenye Baraza la Usuluhishi wa Ndoa au chombo kingine kinachotambulika kisheria.
Wakili Chakila anasema baada ya hapo, pande zote mbili huitwa na kupewa nafasi sawa ya kusikilizwa kwa kuzingatia kanuni ya haki inayosema kuwa hakuna mtu anayepaswa kuhukumiwa bila kusikilizwa.
Anasema pale inapohitajika, vyombo vya usuluhishi vinaweza kufanya uchunguzi wa kina na kuwaita mashahidi au watu wenye taarifa muhimu ili kusaidia kufikia ukweli na kupata suluhisho la haki.
"Jukumu letu si kutoa adhabu bali kufanya kila jitihada za kuwapatanisha wanandoa na kurejesha maelewano ndani ya familia," anasema.
Amefafanua kuwa usuluhishi unaweza kuzaa matokeo mawili endapo utafanikiwa, Baraza la Usuluhishi huandaa kumbukumbu rasmi zinazoonyesha kuwa wanandoa wamepatana na wanaendelea kuishi pamoja kwa amani.
Wakili Chakila anafafanua kuwa iwapo usuluhishi hautafanikiwa, baraza hutoa hati ya kuthibitisha kuwa jitihada zote zimefanyika bila mafanikio, na hati hiyo humruhusu mhusika kufungua shauri mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria, ikiwemo kuomba talaka endapo ataona inafaa.
Anaongeza kuwa hata shauri linapofikishwa mahakamani mahakama huendelea kuzingatia misingi ya haki kwa kuwasikiliza wahusika,kupokea ushahidi na, pale inapowezekana, kuhimiza maridhiano kabla ya kutoa uamuzi wa mwisho.
ATHARI ZA MIGOGORO KWA WATOTO
Akizungumzia athari za migogoro ya ndoa kwa watoto, Chakila anasema watoto ndio waathirika wakubwa wa migogoro na kuvunjika kwa familia.
Anaeleza kuwa wazazi wanapoachana, mara nyingi mtoto hukosa fursa ya kulelewa na wazazi wote wawili na wakati mwingine hulazimika kuishi na mzazi wa kambo au mlezi mwingine, jambo linaloweza kumfanya akose upendo, uangalizi na malezi anayoyahitaji.
Kwa mujibu wa Wakili huyo , mazingira hayo yanaweza kuathiri maendeleo ya mtoto kisaikolojia, kitabia na hata kitaaluma, ndiyo maana Wizara inaendelea kuhimiza migogoro ya kifamilia kutatuliwa kwa njia ya mazungumzo na maridhiano ili kulinda maslahi ya watoto.
"Watoto wanahitaji malezi ya wazazi wote wawili. Ndiyo maana tunasisitiza migogoro itatuliwe kwa njia ya mazungumzo na maridhiano pale inapowezekana, ili kulinda ustawi wa familia na kuhakikisha kizazi kinachokua kinapata msingi mzuri wa maisha," anasema.
CHANGAMOTO YA UTATUZI
Hata hivyo, Chakila anakiri kuwa usuluhishi wa migogoro ya ndoa hukabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo hisia kali zinazowakumba wanandoa wanaofika kwenye vyombo vya usuluhishi.
Anasema mara nyingi baadhi ya wanandoa hufika wakiwa tayari wameamua kuvunja ndoa na hivyo huwa vigumu kukubali ushauri au maridhiano kwa haraka.
Mkurugenzi Msaidizi huyo anasema Changamoto nyingine, ni uelewa mdogo wa baadhi ya wananchi kuhusu nafasi ya vyombo vya usuluhishi, ambapo baadhi huamini kuwa suluhisho pekee la migogoro ya ndoa ni kwenda mahakamani bila kujua kuwa sheria inasisitiza kwanza matumizi ya usuluhishi.
Kwa mujibu wa Chakila, elimu ya sheria inayotolewa na Wizara inaendelea kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa kutumia njia za maridhiano ili kupunguza migogoro, kulinda ndoa na kuimarisha mshikamano wa familia.
DHANA YA TALAKA
Akizungumzia dhana talaka kuongezeka nchini, anasema hali hiyo si lazima ionyeshe kuongezeka kwa migogoro ya ndoa bali imechangiwa zaidi na kuongezeka kwa uelewa wa wananchi kuhusu taratibu rasmi za kushughulikia migogoro hiyo.
Anasema Serikali imeendelea kuhamasisha matumizi ya mabaraza ya usuluhishi kabla ya mashauri kupelekwa mahakamani, hivyo wananchi wengi sasa wanafuata utaratibu huo wa kisheria.
Anaongeza kuwa maamuzi ya mashauri ya ndoa yanayotolewa mahakamani huingizwa katika mfumo rasmi wa Serikali kwa kushirikiana na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), jambo linalosaidia kuwa na takwimu sahihi na kumbukumbu za mashauri hayo.
Wakili huyo anasema wakati mwingine inaweza kuonekana kana kwamba talaka zimeongezeka, ilhali kilichoongezeka zaidi ni matumizi ya mifumo rasmi ya kisheria na uelewa wa wananchi kuhusu haki na taratibu za kushughulikia migogoro ya ndoa.
"Msimamo wa Wizara ya Katiba na Sheria unabaki kujenga jamii inayotatua migogoro kwa mazungumzo, maridhiano na usuluhishi badala ya migongano.
Kupitia utamaduni huo, Serikali inaamini kuwa ndoa nyingi zitaokolewa, watoto watapata malezi bora, familia zitadumu katika amani na mshikamano, na Taifa litaendelea kujenga jamii yenye ustawi na maendeleo endelevu.



0 Comments