Na Asha Mwakyonde, DAR ES SALAAM
UBUNIFU, weledi wa kitaalamu na uwezo wa kuwasilisha fursa za uwekezaji katika sekta ya majengo umeifanya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kuibuka mshindi wa nafasi ya pili na kutunukiwa tuzo ya Banda Bora katika Sekta ya Miliki na Real Estate kwenye Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es salaam (DITF), 'Sabasaba'.
Tuzo hiyo imetolewa wakati wa hafla ya kufunga maonesho hayo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, ambapo kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch. Daud Kondoro, imepokelewa na Mkurugenzi wa Huduma Saidizi wa wakala huo, Amina Lumuli.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 13, 2026, Lumuli amesema mafanikio hayo yametokana na maandalizi makini ya banda la TBA, ubunifu uliotumika pamoja na namna taasisi hiyo ilivyoweza kuwasilisha kwa ufanisi fursa mbalimbali za uwekezaji kwa wananchi na wadau wa maendeleo waliotembelea maonesho hayo.
Amesema kupitia ushiriki wa wakala huo katika maonesho hayo TBA imelenga zaidi kutoa elimu kwa wananchi kuhusu fursa za uwekezaji katika sekta ya majengo, hususan kupitia mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP), ambao unaendelea kutumika katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati.
“Tumekuwa tukitoa elimu kuhusu miradi tunayotekeleza pamoja na fursa zilizopo kwa wawekezaji kushirikiana nasi kupitia mfumo wa PPP ili kuongeza kasi ya maendeleo katika sekta ya ujenzi na majengo,” amesema Lumuli.
Ameeleza kuwa miongoni mwa miradi iliyovutia wananchi wengi waliotembelea banda la TBA ni ujenzi wa nyumba za gharama nafuu, ujenzi wa majengo ya Serikali, pamoja na ukarabati na uboreshaji wa miundombinu ya michezo ikiwemo Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Kwa mujibu wa Lumuli, miradi hiyo inaendelea kuonesha uwezo wa TBA katika kusimamia utekelezaji wa miradi mikubwa ya ujenzi, kutoa suluhisho za kihandisi na kuchangia katika ukuaji wa sekta ya majengo nchini.
Amesema tuzo hiyo ni ishara ya kutambuliwa kwa jitihada za TBA katika kutoa huduma bora, kutumia ubunifu wa kihandisi na kutekeleza miradi yenye mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa.
Aidha, amewataka wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kutumia fursa zilizopo kupitia miradi ya ubia inayotekelezwa na TBA ili kushirikiana katika kujenga miradi yenye tija kwa uchumi wa Taifa.
Hafla ya utoaji wa tuzo na kufungwa kwa Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba iliongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ambapo TBA ilitajwa miongoni mwa taasisi za Serikali zilizofanya vizuri katika utoaji wa huduma, ubunifu na uhamasishaji wa uwekezaji nchini.



0 Comments