KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA AFYA NA MASUALA YA UKIMWI YAIPONGEZA OFISI YA WAZIRI MKUU


Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI Mhe. Stanslaus Nyongo (wa kwanza kulia) akisikiliza maelezo kutoka kwa mmoja wa wanakikundi wa kikundi cha Sitetereki Kata ya Old Shinyanga wanaojishughulisha na utengenezaji wa bidhaa mbalimbali wakati za ziara ya Kamati hiyo mkoani Shinyanga.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga (wa pili kulia) akiangalia vyungu vinavyotengenezwa na Mabinti balehe na wanawake vijana kupitia kikundi cha Tunaweza kilichopo Kata ya Kolandoto, Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga wakati za ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI mkoani Shinyanga.

Baadhi ya Mabinti balehe na wanawake vijana kupitia kikundi cha Tunaweza kilichopo Kata ya Kolandoto Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga  wakionesha namna vyungu vinavyotengenezwa wakati za ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI mkoani Shinyanga.

Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI Mhe. Stanslaus Nyongo akizungumza na baadhi  ya Mabinti balehe na wanawake vijana wakati za ziara ya Kamati hiyo  mkoani Shinyanga.

Baadhi ya Mabinti balehe na wanawake vijana kupitia kikundi cha Tunaweza  na Sitetereki wakifuatilia ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI mkoani Shinyanga.

Baadhi ya Mabinti Balehe na Wanawake Vijana kupitia kikundi cha Jahazi Kata ya Ibadakuli, Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga wakionesha namna ya utengenezaji wa Sabuni za vipande mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI ilipofanya ziara ya kutembelea vikundi mkoani Shinyanga.

(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)

Na Mwandishi wetu- Shinyanga

KAMATI ya kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI imeipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) kwa mafanikio makubwa katika kutekeleza afua za VVU na UKIMWI nchini.

Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Stanslaus Nyongo wakati kamati ilipofanya ziara ya kutembelea na kukagua Mpango wa Dreams kupitia Mradi wa Epidemic Control (EPIC) unaotekelezwa na Shirika la Family Health International (FHI360) kwa wasichana balehe na wanawake vijana (AGYW) katika katika Mkoa wa Shinyanga.

Akizungumza mara baada ya kukagua vikundi vya vijana  vikiwemo  Sitetereki kilichopo Kata ya Old Shinyanga, Jahazi, Kata ya Ibadakuli na Tunaweza katika Kata ya Kolandoto Mhe. Nyongo amesema lengo la ziara ni kujionea maendeleo ya mradi huo na kuishauri Serikali maeneo ya kuboresha ili kuendeleza jitihada za kuwa na vijana wenye afya nzuri wanaoshiriki katika shughuli za uzalishaji na kujiletea maendeleo yao.

“Tunapongeza kazi kubwa inayofanywa na Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kutoa maelekezo ya kumlinda mtoto wa kike hasa  katika  gonjwa kubwa la  UKIMWI, namna ya kumkomboa mtoto wa kike, kujifunza kazi za ujasiliamali ili kujikwamua katika maisha pamoja  kupaza sauti dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia hivyo sisi kama wabunge tumeridhishwa na kazi inayofanywa na Serikali,”Amesema Mwenyekiti huyo.

Naye Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga amewaomba vijana wa kike kuendelea kujiamini na kufanya kazi vizuri kwani Serrikali ya Awamu ya Sita inawajali vijana na kutambua mchango wao mkubwa katika maendeleo ya Taifa.

Akizungumzia ziara hiyo  Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI Mhe. Hassan Mtenga  ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha za kukamilisha na kujengwa kwa miradi mikubwa ya maendeleo huku akiipongeza TACAIDS na wadau wa maendeleo kuwa na mwamko wa kuwawezesha vijana kujikwamua kiuchumi.

“Tumejifunza kitu kwasababu  tunao watu wako tayari kupiga vita janga  kuu la UKIMWI na niishukuru TACAIDS, Mawaziri wenye dhamana na hawa wadada ambao  wameamua kutoka kwenye  sughuli za kuuza bar na kuanzisha biashara  zao sasa uwe mfano  wa kuigwa kwa maeneo mengine,”amepongeza Mhe. Mtenga.

Vilevile Mjumbe wa Kamati hiyo Mhe. Christina Mnzava amesema wazazi na walezi wana wajibu wa kusimamia malezi sahihi ya watoto ili kuwakomboa katika tabia hatarishi huku  akiupongeza Mpango wa Dream kwa kuamua  kuwafikia mabinti katika maeneo yao akishauri mradi huo kuongeza wigo na kuwafikia vijana wengine  waliopo Vijijini .

“Sisi kama wazazi na walezi tunaweza kuwakomboa watoto wetu katika tabia hatarishi ambazo wanazipata mtaani kuna wengine walikuwa wanauza miili yao, lakini kutokana na mradi huu wamejikwamua wamefundishwa ujasiriamali, kuwekeza tumeona wasichana wamejitambua wanatengeneza sabuni, batiki, vyungu katika vikundi vya  Kata za Old Shinyanga, Ibadakuli na Kolandoto kwa kweli wamefanya vizuri,”Ameeleza Mjumbe huyo.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe Christina Mndeme amesema Serikali ipo tayari kushirikiana na Mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kuondoa unyanyapaa na ubaguzi kwa watu wanaoishi na VVU ambao upo juu, kuwajengea vijana uwezo wa kiuchumi ili muda mwingi wautumie kwenye uzalishaji na sio kwenye mambo yanayoweza kuwasababishai maambukizi ya VVU,kuelimisha jamii kuacha mila potofu ambazo zinasababisha ukatili wa kijinsia.

Kwa upande wake Mshauri Mwandamizi wa Mpango wa Dreams kupitia Mradi wa Epidemic Control (EPIC) unaotekelezwa na Shirika la Family Health International (FHI360) Bi. Agnes Junga amefafanua kuwa lengo la Mpango huo ni kupunguza maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kwa wasichana  kuanzia umri wa miaka Tisa hadi 24.

“Mpango huu ulizinduliwa 2014 ukilenga kupunguza maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwa Nchi 13 za Bara la Afrika ikiwemo Tanzania ambapo tulianza na Halmashauri Sita  na hadi sasa tumefikia Halmashauri 12. Shirika la (FHI360) kwenye mradi wa EPIC tunatekeleza  Dreams  katika Mikoa miwili ya Shinyanga  ndani ya Halmashauri Tano na Iringa katika Halmashauri mbili na tunawafikia wasichana kuanzia miaka 15 hadi 25 walio nje ya shule pamoja na wazazi au walezi na jamii kwa ujumla  tuhakikishe msichana anafikia ndoto zake.

Aidha akizungumza  kwa niaba ya wanakikundi kutoka Vikundi vya Mabinti Balehe na Wanawake Vijana vya Sitetereki, Tunaweza na Jahazi mwanakikundi Sungi Leonard amesema uanzishwaji wa vikundi  hivyo vimewasaidia kama mabinti kujitambua, kufahamu elimu ya afya, kuwajengea uwezo wa kukabiliana na vitendo vya kikatili pamoja na kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi mapya ya VVU na kuwawezesha kiuchumi .

“Nilikutana na mwezeshaji kiuchumi na mwelimishaji rika  nikapata elimu ya ukatili wa kijinsia, umuhimu wa upimaji wa  afya, matumizi sahihi ya kinga, magonjwa ya ngono  na VVU ambayo imenisaidia kujitambua kama binti. Pia nilifanikiwa kujiunga katika kikundi cha Sitetereki nikajifunza kutengeneza batiki kazi ambayo inanipatia kipato na ninamudu mahitaji yangu tofauti na ilivyokuwa awali,”Ameshukuru Mwanakikundi huyo.

Post a Comment

0 Comments

MAJALIWA: MJI KONDOA TUMEKUSANYA ZAIDI YA MILIONI 126 KIPINDI CHA JULAI HADI JUNI MWAKA HUU