NACTVET YAONESHA MATUNDA YA ELIMU YA AMALI SABASABA


Na Asha Mwakyonde, DAR ES SALAAM

BARAZA la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) limewataka wananchi kutumia fursa ya Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) kutembelea banda lake ili kupata taarifa sahihi kuhusu elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, sambamba na kujionea mafanikio ya utekelezaji wa mkondo wa elimu ya amali unaoendelea katika shule mbalimbali za sekondari nchini.

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko wa NACTVET, Dora Tesha, amesema maonesho hayo yameipa taasisi hiyo nafasi ya kukutana ana kwa ana na wananchi, wanafunzi na wadau mbalimbali ili kuwafahamisha huduma zinazotolewa pamoja na mchango wa elimu ya ufundi katika kukuza ujuzi na ajira kwa vijana.

Amesema kupitia banda la NACTVET, wananchi wanapata maelezo kuhusu vyuo vinavyotambuliwa na Baraza, programu za masomo zilizoidhinishwa, utaratibu wa kuomba nafasi za masomo, pamoja na huduma za usajili wa vyuo vipya vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi.

"Tunatoa pia huduma kwa wanaohitaji vyeti vya matokeo ya masomo na ushauri kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na NACTVET. Tunawahimiza wananchi kutembelea banda letu ili wapate taarifa sahihi na huduma kwa wakati," amesema Tesha.

Ameongeza kuwa moja ya vivutio vikubwa katika maonesho ya mwaka huu ni ushiriki wa wanafunzi wanaosoma mkondo wa elimu ya amali, ambao wanaonesha kwa vitendo ubunifu na ujuzi walioupata kupitia mfumo huo wa elimu.

Kwa mujibu wa Tesha, mkondo wa elimu ya amali umetokana na maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, toleo la mwaka 2023, ambayo inalenga kuwajengea vijana maarifa na ujuzi unaowawezesha kujiajiri au kuajiriwa baada ya kuhitimu masomo.

Amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika elimu inayozingatia ujuzi ili kuwaandaa vijana kukabiliana na mahitaji ya soko la ajira la sasa na la baadaye.

Kwa upande wake, mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Bwiru Boys, Daudi Elias, amesema kusoma mkondo wa elimu ya amali kumembadilishia mtazamo na kumpa ujuzi unaomwezesha kujitegemea pamoja na kujiandaa kwa maisha ya baadaye.

Amesema mfumo huo unawapa wanafunzi nafasi ya kujifunza kwa vitendo na kupata stadi zinazoweza kuwasaidia kujiajiri hata kabla ya kuendelea na elimu ya juu.

Daudi ameishauri Serikali kuendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa kuongeza walimu wa masomo ya amali, vitabu pamoja na vifaa vya kufundishia ili wanafunzi wengi zaidi wanufaike na mfumo huo unaozingatia ujuzi na ubunifu.

Naye mwanafunzi wa Kidato cha Tatu katika Shule ya Sekondari Baobab jijini Dar es Salaam, Caren Mark, anayesoma mkondo wa elimu ya amali katika fani ya Electrical Installation, amesema amechaguliwa na NACTVET kushiriki maonesho hayo kwa lengo la kuonesha kazi za ubunifu zinazofanywa na wanafunzi.

Caren amesema katika banda la NACTVET anaonesha mradi wa mfumo wa vifaa vya umeme vya majumbani unaojumuisha kengele za usalama, taa zinazowashwa kwa mfumo wa sensor wakati wa giza na teknolojia nyingine zinazoweza kutumika katika nyumba, shule, hospitali na maeneo mbalimbali.

Amesema elimu ya amali imemwezesha kubuni na kutengeneza mifumo hiyo, huku akiwahimiza wasichana kujitokeza kwa wingi kusomea fani za ufundi kwa kuwa zinatoa fursa nyingi za ajira, ubunifu na kujiajiri.

Post a Comment

0 Comments

CFR YATAKA VIJANA KUTUMIA FURSA ZA DIPLOMASIA YA UCHUMI