Na Asha Mwakyonde, TANGA
CHUO Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kimeweka historia kwa kushiriki kwa mara ya kwanza katika Tuzo za Watafiti Waliochapisha Matokeo ya Tafiti Zao katika Majarida yenye Hadhi ya Juu Kimataifa, zinazotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (MoEST).
Hatua hiyo imekuja baada ya Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo hicho Mhandisi Dk. Abdulrahim Haroun Ali Suleiman, kufanikiwa kutwaa tuzo hiyo, jambo linaloashiria kuimarika kwa tafiti na uchapishaji wa matokeo ya tafiti za watafiti wa Chuo hicho katika majarida ya kimataifa yenye hadhi ya juu.
Hayo yamesemwa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi, Profesa Abdi Talib Abdalla, wakati akitoa maelezo kwa
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia nchini, Profesa Adolf Mkenda alipotembelea banda la Chuo hicho katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara jijini Tanga, wakati wa Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu.
Amesema mafanikio hayo ni hatua muhimu katika safari ya Chuo ya kuimarisha utafiti na kuongeza mchango wa tafiti katika maendeleo ya Taifa.
Prof. Abdi Talib ameongeza kuwa ushiriki wa SUZA katika tuzo hizo kwa mara ya kwanza unaonesha hatua inayopigwa na Chuo katika kujenga mazingira yanayowezesha watafiti kufanya tafiti zenye ubora na kuchapisha matokeo yake katika majarida yanayotambulika kimataifa.
Ameelza kuwa katika Wiki hiyo ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu, SUZA inaendelea kutambulisha programu mpya za kitaaluma, zikiwemo Shahada ya Kwanza ya Akili Unde na Sayansi ya Data (Bachelor of Artificial Intelligence and Data Science) pamoja na Shahada ya Kwanza ya Usimamizi wa Usafirishaji na Uendeshaji wa Bandari (Bachelor of Shipping and Port Logistics Management).
Mbali na programu hizo, amefafanua kuwa Chuo hicho kimeonesha bunifu mbalimbali zinazolenga kutumia teknolojia kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi, ikiwemo mfumo wa uuzaji wa samaki mtandaoni, mfumo wa kugundua changamoto chini ya ardhi, mfumo wa ufuatiliaji wa afya pamoja na bunifu za ujasiriamali.
Amesema, Ushiriki huo unaendelea kukazia nafasi ya SUZA katika kuendeleza elimu, utafiti, ubunifu na ujuzi, huku ukionesha namna taasisi za elimu ya juu zinavyoweza kutumia maarifa na teknolojia katika kutengeneza suluhisho na kuchochea maendeleo ya Taifa.

0 Comments