Na Asha Mwakyonde, DODOMA
BARABARA bora ni kiungo muhimu kati ya uzalishaji na masoko, huku usalama wa miundombinu ukitegemea ubora wa ujenzi na matengenezo yake.
Kwa kutambua umuhimu huo, Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA),umeendelea kuboresha mtandao wa barabara, madaraja na makalavati, sambamba na kuimarisha huduma za kitaalamu za upimaji wa udongo na vifaa vya ujenzi.
Akizungumza leo Agosti 8, 2026 katika Maonesho ya Nanenane yanayofanyika katika Viwanja vya Dk. John Malecela, Nzuguni jijini Dodoma, Mhandisi kutoka Ofisi ya Meneja wa TARURA Mkoa wa Dodoma, Revocatus Nsubile, amesema taasisi hiyo inasimamia mtandao wa barabara wenye urefu wa kilomita 144,429.78 nchini, unaojumuisha barabara za lami, changarawe na udongo.
Amesema barabara hizo ni muhimu katika kurahisisha usafirishaji wa mazao kutoka mashambani kwenda masokoni, hivyo kuchangia shughuli za kiuchumi na maendeleo ya wananchi.
DODOMA YANUFAIKA NA MIRADI
Mhandisi Nsubile amesema katika mwaka wa fedha 2025/26, TARURA Mkoa wa Dodoma imejenga madaraja makubwa 53 ya zege, madaraja ya mawe 50, box culverts 106 pamoja na kuweka pipe culverts zenye urefu wa mita 4,356.
Aidha, ameeleza kuwa taa 1,268 zimefungwa katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo kwa lengo la kuongeza usalama wa watumiaji wa barabara wakati wa usiku.
Mhandisi huyo akizungumzia Dodoma Jiji, amesema TARURA imejenga madaraja makubwa matatu ya zege na matatu ya mawe, huku madaraja 17 ya zege ya ukubwa wa kati yakijengwa katika maeneo mbalimbali.
Amefafanua kuwa daraja la mawe lililojengwa katika eneo la Kikuyu litasaidia kurahisisha usafiri wa wananchi wanaoelekea Chuo Kikuu cha Dodoma na Hospitali ya Benjamin Mkapa, huku daraja jingine likijengwa eneo la Mpombo kuelekea Msisi.
Katika hatua nyingine, ameeleza kuwa TARURA imeweka pipe culverts zenye urefu wa mita 698 na kufunga taa 352 katika Dodoma Jiji.
MIRADI YA 2026/27
Akizungumzia mipango ya mwaka wa fedha 2026/27, Mhandisi Nsubile amesema TARURA itaendelea kuboresha barabara za lami katika maeneo mbalimbali ya Dodoma.
Amesema barabara ya Ziguli hadi Mahamanyika yenye urefu wa kilomita 5.5 itaongezewa takribani kilomita mbili, hatua inayolenga kuboresha mawasiliano na kutoa njia mbadala kwa wananchi wanaoelekea Mji wa Serikali.
Mhandisi Nsubile amesema ujenzi wa barabara katika eneo la Nzuguni Link utaendelea kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha, huku maandalizi ya usanifu yakiwa yamefanyika.
VIPIMO KULINDA UBORA WA UJENZI
Mbali na miundombinu ya barabara, amebainisha kuwa TARURA imeendelea kutoa huduma za kitaalamu za upimaji wa udongo na vifaa vya ujenzi kwa taasisi na wananchi binafsi.
Naye Mhandisi wa Vifaa na Maabara wa TARURA, Emmanuel Kilasi, amesema wananchi wanashauriwa kufanya vipimo vya udongo na vifaa vya ujenzi kabla ya kuanza ujenzi ili kubaini ubora na uwezo wa eneo husika kubeba jengo.
Amesema huduma hiyo inahusisha upimaji wa vifaa kama mchanga, kokoto, nondo na zege, pamoja na uchunguzi wa udongo kwa lengo la kutoa ushauri kuhusu aina ya msingi inayofaa.
“Tunawakaribisha watu wote, wawe wajenzi, taasisi au wananchi, kuleta maeneo yao kupimiwa udongo kabla ya ujenzi. Pia wanaweza kuleta vifaa vya ujenzi kama kokoto na mchanga kupimwa ili kujua kama vina sifa zinazohitajika,” amesema.
Ameeleza kuwa baadhi ya maeneo yana udongo wenye changamoto, ikiwemo problematic soil, ambao unaweza kushika maji, kutanuka unapolowa na kusinyaa unapokauka, hali inayoweza kusababisha nyufa katika majengo au barabara endapo hatua za kitaalamu hazitachukuliwa.
Amesema TARURA pia hutumia vifaa kama Rebound Hammer kupima uimara wa zege na kuthibitisha kama limefikia kiwango kinachohitajika.
CBRM KUONGEZA AJIRA NA KULINDA BARABARA
Kwa upande wake, Mratibu wa Mpango wa Matengenezo Endelevu ya Barabara kwa Kushirikisha Jamii (CBRM), Mhandisi Richard Missa, amesema TARURA inapanga kupanua mpango huo katika mikoa 25 mwaka wa fedha 2026/27.
Amesema CBRM unashirikisha vikundi vya kijamii vinavyoishi karibu na barabara katika kufanya matengenezo ya kawaida, ikiwemo kuzibua makaravati na madaraja, kuondoa udongo na vipande vya miti barabarani pamoja na kukata nyasi.
Amesema mpango huo ulianza mwaka 2021 na katika hatua ya awali zaidi ya kilomita 150 za barabara zilifanyiwa matengenezo kwa kushirikisha vikundi vya jamii.
“Lengo ni kutunza barabara zetu, lakini pia kuongeza kipato cha wananchi na kuwajengea hisia ya umiliki wa barabara wanazozitumia,” amesema.
Ameongeza kuwa mwaka 2026/27 mpango huo unalenga kufikia zaidi ya halmashauri 104, huku vikundi vya jamii vikiendelea kupewa mafunzo na fursa za kushiriki katika mikataba ya matengenezo.
Mhandisi Missa amesema CBRM unatarajiwa kuendelea kuwa sehemu ya shughuli za TARURA hata baada ya kukamilika kwa kipindi cha mradi, kutokana na umuhimu wake katika kupunguza uharibifu wa barabara na gharama za matengenezo makubwa.
TARURA imeeleza kuwa uwekezaji katika barabara, matumizi ya teknolojia za upimaji na ushirikishwaji wa jamii ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha miundombinu inakuwa salama, imara na yenye kusaidia shughuli za uzalishaji na biashara kwa wananchi.





0 Comments