DAR ES SALAAM
WANANCHI wa Mtaa wa Mpakani, Kata ya Saranga, wameanza kupata matumaini mapya ya kusogezewa huduma za afya baada ya Diwani wa Kata hiyo, John Sanga, kuunda Kamati Maalum ya kusimamia ujenzi wa zahanati katika eneo hilo.
Hatua hiyo imekuja baada ya mkutano kati ya Diwani Sanga na wananchi wa Mtaa wa Mpakani, ambapo wananchi walipata fursa ya kueleza changamoto mbalimbali zinazowakabili, ikiwemo upatikanaji wa maji, ulinzi shirikishi, huduma za afya na miundombinu ya barabara.
Akizungumza Agosti 23, 2026 katika Mkutano huo ulioandaliwa na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Saranga, Leonard Mbangile ambao ulilenga kujadili utekelezaji wa miradi ya maendeleo na namna ya kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
ZAHANATI MPAKANI
Ameeleza kuwa katika hatua ya kuboresha huduma za afya, Diwani Sanga aliendesha harambee maalum kwa ajili ya kuanza ujenzi wa zahanati katika Mtaa wa Mpakani, ambapo wananchi walichangia zaidi ya tofali 3,000 kwa ajili ya kuanzisha ujenzi huo.
Sanga pia ameunda Kamati Maalum ya Ujenzi itakayokuwa na jukumu la kusimamia na kuratibu shughuli zote za ujenzi wa zahanati hiyo.
Kwa mujibu wa Mhandisi Sanga eneo la ujenzi tayari limetengwa, huku michoro pamoja na kibali cha ujenzi vikiwa tayari. Ujenzi unatarajiwa kufanyika kwa kushirikisha nguvu za wananchi, kwa lengo la kusogeza huduma za afya karibu na wananchi wa Mtaa wa Mpakani.
MAJI
Akizungumzia kuhusu changamoto ya maji, Diwani Sanga amemtaka Mhandisi Gabriel kutoka DAWASA, aliyeshiriki katika mkutano huo, kufuatilia na kutatua changamoto ya maji katika maeneo yanayohusika.
Aidha, ameitaka DAWASA kuweka ratiba maalum ya mgao wa maji ili wananchi waweze kufahamu siku na muda ambao huduma hiyo itapatikana.
ULINZI SHIRIKISHI
Katika kuimarisha usalama wa wananchi, Diwani Sanga amewaomba Mabalozi wa Mtaa kuandaa vijana 25 ambao watapatiwa mafunzo maalum ya ulinzi shirikishi.
Mhandisi Sanga ameahidi kushirikiana na wahusika kuhakikisha vifaa muhimu vya ulinzi vinapatikana sambamba na mafunzo kwa vijana watakaoshiriki katika shughuli hizo.
BARABARA
Mhandisi Sanga amewahakikishia wananchi kuhusu miundombinu ya barabara, kuwa juhudi zinaendelea kutatua changamoto.
Amesema kazi zinaendelea katika Barabara ya Msingwa, ikiwemo uwekaji wa zege katika maeneo korofi na ujenzi wa madaraja, huku Baraza la Kata likiwa limebainisha barabara zote zinazohitaji matengenezo ndani ya Kata ya Saranga.
Aidha, barua ya kuomba grela kutoka Manispaa tayari imewasilishwa, na Kata ya Saranga inatarajiwa kupatiwa grela kwa ajili ya kuchonga na kuboresha barabara mbalimbali.
USHIRIKIANO NA MBUNGE
Katika mkutano huo, Diwani Sanga amemshukuru Mbunge Angellah Kairuki kwa ushirikiano katika kushughulikia kero na changamoto zinazowakabili wananchi wa Kata ya Saranga.
Amesisitiza kuwa ushirikiano huo utaendelea kuimarishwa ili kuhakikisha changamoto za wananchi zinasimamiwa kwa karibu na kupatiwa ufumbuzi kwa wakati.



0 Comments