DASPA YAHAMASISHA WAKULIMA KULIMA MBEGU YA MTAMA AINA YA TARISOR1

Na Asha Mwakyonde, Dodoma 

WAKULIMA wa zao la mtama wameshauriwa kutumia mbegu ya mtama aina ya TARISOR1 kwa kuwa mtama huo hauliwi na ndege kama ilivyo kwa mtama mwingine.

Akizungumza leo Agosti 3,2024 Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Wakulima Wazalishaji Mbegu Dodoma (DASPA) Aithan Chaula katika maonesho ya wakulima na Wafugaji (Nane nane), ambayo yanafanyika Kitaifa viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma amesema shirika hilo linazalisha aina nne za mbegu bora ambazo ni mtama, uwele, mbaazi, karanga na kunde.

Akizungumzia zao la mtama amesema zao hilo lina fanya vizuri katika Mkoa wa Dodoma ambalo linakwenda sambamba na hali ya hewa iliyopo katika Mkoa huo.

Mkurugenzi Mtendaji huyo ameeleza kuwa mtama huo unafaida katika mwili wa binadamu na unampatia mkulima kipato cha uhakika.

Amesema aina hiyo ya mtama ni mzuri kwa lishe na kwamba unasaidia watu kutokuzeeka pindi anapokunywa uji wake asubuhi na baadae ugali mchana au jioni.

Chaula ameeleza kuwa Shirika hilo linahakikisha mkulima anazalisha mbegu ngazi ya mkulima, ambazo anawauzia wakulima wengine kwa bei nafuu ambayo mkulima anaweza kumudu gharama tofauti na ambavyo wananunua.

"Katika kuhakikisha hilo DASPA imejikita kuzalisha mbegu takribani nne ambazo ni karanga ambazo zimegawanyika katika makundi manne Nachi 2015, Tanzanut 2016, Naliendele 2016 na NARINUT 2015," amesema Chaula.

Amefafanua kuwa hizo ni aina za karanga ambazo zinavumilia mabadiliko ya tabia nchi pamoja na magonjwa.

Mkurugenzi Mtendaji huyo ameeleza kuwa mbegu hizo za karanga hazina magonjwa mengi kama ilivyozoeleka na zina mafuta mangi na lishe ya kutosha.

" DASPA haijaishia hapo kwenye zao hili la karanga imehakikisha mkulima anaweza kuongeza mnyororo wa thamani kwenye zao hili badala ya kuuza kama karanga," amesema.

Ameongeza kuwa wana mbegu ya zao la mbaazi ambayo ni Ilonga14 M2 kwa Mkoa wa Dodoma inafanya vizuri na inaanza kuzaa mwezi wa tatu hadi wa sita.

"Mkulima anaweza kuvuna kwa muda wa miezi sita. Wakati wa mvua inaendelea kukua kwa ajili ya mwaka wa pili itaendea kuvunwa bila kupanda nyingine, zao hili lina faida na linasaidia udogo kuendeIea kuwa na rutuba kwa kuwa mizuzi yake inakwenda mbali kutafuta maji, " ameeleza Chaula.

Ameongeza kuwa zao hili lina faida kwa mkulima kwani, atatumia kwa chakula na biashara ambapo mwaka huu kilogramu moja inauzwa 3000.

Akizungumzia zao la kunde amesema kuwa zao hilo linaweza kulimwa wakati wowote masika na kiangazi endapo itamwagiliwa na kwamba linafanya vizuri zaidi wakati ambapo hakuna mvua nyingi.

Post a Comment

0 Comments

 MAGARI 25 YA TUME YA MADINI YAMEZINDULIWA,YATASAMBAZWA KWENYE OFISI ZA MAAFISA MADINI